Tukitokea katika sharti ya pili aliyotaja (Rahimahu Allaah) tunasema yafuatayo: njia za kulingania kwa Allaah ni jambo la kukomeka. Hakutakiwi kuzuliwa kitu ambacho Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) alikuwa hakifanyi. Ndio maana Salaf waliwakaripia kwelikweli waimbaji, kitu kilichokuwa kinafanywa na Suufiyyah. Haijalishi kitu hata kama nyimbo hizi zimesalimika na zana za haramu, zana za nyimbo na mengineyo. Haijalishi kitu hata kama nyimbo hizi zinalainisha mioyo. Walifanya hivo si kwa jengine ni kwa sababu mambo haya hayana ushahidi katika Qur-aan, Sunnah wala matendo ya Salaf (Radhiya Allaahu ´anhum). Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema katika “Majmuu´-ul-Fataawaa”:

“Ama zile nyimbo za wale wenye kukusanyika huku wakikusudia kuzitengeneza nyoyo na kuzitakasa nyoyo zao, wakaimba pasi na zana za nyimbo, mfano wa kile kinachoitwa “Ghubaar”, kupiga makofi na mfano wake, ni nyimbo zilizozuliwa ndani ya Uislamu. Ni jambo limezuliwa baada ya kupita karne tatu ambao Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewasifu pale aliposema:

“Karne bora ni ile niliyotumilizwa kwayo, kisha ile itakayofuatia, kisha ile itakayofuatia.”[1]

Ni jambo limechukizwa na wale watu muhimu wa Ummah na hawakuyadhuhuria wanachuoni wakubwa.”[2]

Mpaka pale ambapo Shaykh alisema:

“Kwa kufupisha ni kwamba muumini anatakiwa kutambua kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuacha jambo lolote linalomkurubisha mtu na Pepo isipokuwa alilisimulia. Na wala hakuacha chochote kinachomuweka mtu mbali na Moto isipokuwa alikisimulia. Nyimbo hizi iwapo zingelikuwa na manufaa basi zingeliamrishwa na Allaah na Mtume Wake. Kwani Allaah (Ta´ala) amesema:

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا

 “Leo wamekata tamaa wale waliokufuru juu ya dini yenu, hivyo basi msiwaogope na niogopeni Mimi. Leo nimekukamilishieni dini yenu na nimekutimizieni neema Yangu na nimekuridhieni Uislamu uwe dini yenu.”[3]

Ingelikuwa na manufaa moyoni mwake na wakati huohuo kitu hicho kikawa hakina ushahidi kutoka katika Qur-aan wala Sunnah, basi kitapuuzwa. Sahl bin ´Abdillaah at-Tusturiy amesema:

“Kila kitu ambacho mtu anakihisi moyoni mwake kisichokuwa na ushahidi katika Qur-aan na Sunnah basi kitu hicho ni batili.”

ad-Daaraaniy amesema:

“Wakati mwingine mimi nahisi moyoni mwangu nukta ya kielimu na siikubali mpaka kwa mashahidi wawili ambao ni waadilifu; Qur-aan na Sunnah… “[4]

Maneno yake aliposema:

“Ingelikuwa na manufaa moyoni mwake na wakati huohuo kitu hicho kikawa hakina ushahidi kutoka katika Qur-aan wala Sunnah.”

kuna Radd yenye nguvu juu ya wale waliojuzisha filamu kwa ajili ya kulingania katika dini ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Hoja yao eti kuna manufaa na kwamba nyoyo hulainika pindi wanapozisikiliza na kuzitazama.

Kujengea juu ya hayo tunasema kuwa ni lazima njia za Da´wah ziwe zimetokana na dalili ya Qur-aan na Sunnah. Kusifanywe ndani yake isipokuwa yale yaliyofanywa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake watukufu.

[1] al-Bukhaariy (2652) na Muslim (2533).

[2] Majmuu´-ul-Fataawaa (11/591).

[3] 05:03

[4] Majmuu´-ul-Fataawaa (11/594-595).

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Usuwl-ud-Da´wah as-Salafiyyah, uk. 38-40
  • Imechapishwa: 06/08/2020