12. Msingi wa tatu: kutomkufurisha muislamu yeyote ila kwa kufanya kichenguzi cha Uislamu

Miongoni mwa misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni kwamba hawamkufurishi muislamu yoyote isipokuwa pale atapofanya moja ya vichenguzi vya Uislamu. Kuhusu yule ambaye atafanya dhambi kubwa ambayo iko chini ya shirki na dhambi hiyo isifahamishe ukafiri kwa yule mwenye kuitenda, kama kwa mfano kuacha swalah kwa uvivu, hawamhukumu ukafiri yule ambaye anafanya dhambi kubwa. Badala yake wanamhukumu kutenda dhambi nzito na kwamba imani yake ni pungufu. Asipotubia kwayo, basi yuko chini ya matakwa. Endapo Allaah atataka atamsamehe na akitaka atamuadhibu. Lakini [ikibidi kumuadhibu] hatomdumisha Motoni milele. Amesema (Ta´ala):

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa na anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa amtakae. “[1]

Katika hayo madhehebu ya Ahl-us-Sunnah wako kati kwa kati baina ya Khawaarij ambao wanakafirisha kwa kutenda dhambi kubwa hata kama itakuwa chini ya kufuru na baina ya Murji-ah ambao wanasema kuwa mtu huyo ni muumini mwenye imani kamili. Aidha wanasema kuwa imani haidhuriki kitu ikiambatana na maasi kama ambavyo utiifu vilevile haunufaishi kitu ukiambatana na kufuru.

[1] 04:48

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Min Usuwl ´Aqiydah Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 25-26
  • Imechapishwa: 12/05/2022