16. Msimamo sahihi juu ya mabishano katika dini

Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ahh wanakataza mabishano na magomvi katika dini, kwa kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza hilo. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema:

“Isomeni Qur-aan muda wa kuwa nyoyo zenu zimeshikana juu yake. Mtapotofautiana, basi simameni kutoka kutokamana nayo.”

Katika “al-Musnad” na “as-Sunan” ya Ibn Maajah – msingi wa matamshi yake yanapatikana katika “as-Swahiyh” ya Muslim kutoka kwa ´Abdullaah bin ´Amr – kumesimuliwa:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitoka na wao wakibishana juu ya Qadar. Uso wake ukageuka mwekundu kama mkomamanga kutokana na hasira. Akasema: “Haya ndio mliyoamrishwa au mliumbwa kwa ajili ya haya? Mnaigonganisha sehemu ya Qur-aan na nyingine. Haya ndio yaliwafanya kuangamia nyumati zilizokuwa kabla yetu.”

Imepokelewa vilevile kuwa mabishano ni njia moja wapo ya adhabu ya Allaah juu ya Ummah. Katika “as-Sunan” ya at-Tirmidhiy na Ibn Maajah kumepokelewa kutoka kwa Abu Umaamah (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna watu waliopotea baada ya uongofu waliokuwemo isipokuwa baada ya kuanza mabishano.” Kisha akasoma:

مَا ضَرَبُوهُ لَكَ إِلَّا جَدَلًا

“Hawakukupigia mfano huo isipokuwa tu kutaka kubisha.” (43:58)

Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

“Misingi ya Sunnah kwetu ni kushikamana na yale waliyokuwemo Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kuwaigiliza, kuacha Bid´ah na kila Bid´ah ni upotevu, kuacha magomvi na kukaa na Ahl-ul-Ahwaa´ pamoja na kuacha mizozo, mabishano na magomvi katika dini.”

Yote haya yanahusu yale mabishano ya batili, mabishano ya haki baada ya kuwa haki imeshabainika, mabishano ambayo hoja zake hazitambuliki na yule anayejadiliwa, mabishano juu ya zile Aayah zisizokuwa wazi au mabishano pasi na kuwa na nia nzuri na mfano wa hayo.

Hata hivyo endapo mabishano yatakuwa ni yenye kuhusiana na kuidhihirisha na kuibainisha haki na ikawa ni yenye kubainishwa na mwanachuoni aliye na nia njema na aliyelazimiana na adabu, basi yanazingatiwa kuwa yenye kusifiwa. Allaah (Ta´ala) amesema:

ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ

“Waite watu katika njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mazuri na jadiliana nao kwa njia bora zaidi.”  (16:125)

وَلَا تُجَادِلُوا أَهْلَ الْكِتَابِ إِلَّا بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ

“Na wala msibishane na Ahl-ul-Kitaab isipokuwa kwa yale ambayo ni bora zaidi.” (29:46)

قَالُوا يَا نُوحُ قَدْ جَادَلْتَنَا فَأَكْثَرْتَ جِدَالَنَا فَأْتِنَا بِمَا تَعِدُنَا إِن كُنتَ مِنَ الصَّادِقِينَ

“Wakasema: “Ee Nuuh! Kwa hakika umejadiliana nasi na umekithirisha majadiliano nasi, basi tuletee adhabu unayotutishia nayo ukiwa ni miongoni mwa wakweli.”” (11:32)

Kadhalika Amesimulia (Ta´ala) juu ya mjadala wa Ibraahiym (´alayhis-Swalaatu was-Salaam) pamoja na watu wake na Muusa (´alayhis-Swalaatu was-Salaam) pamoja Fir´awn. Katika Sunnah kumetajwa mabishano ya Muusa na Aadam (´alayhimaas-Swalaatu was-Salaam) kama ambavyo vilevile kumetajwa mabishano mengi kutoka kwa Salaf. Yote haya ni mabishano yenye kusifiwa midhali ndani yake mna elimu, nia njema, yanayoafikiana na Shari´ah na adabu katika kujadiliana.

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Mu´taqad as-Swahiyh, uk. 95-96
  • Imechapishwa: 22/06/2020