12. Maelezo kuhusu Hadiyth ya atakayehuisha katika Uislamu mwenendo mzuri

Isitoshe tunasema kwamba Hadiyth haifahamishi uanzilishi wa kila aina. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Atakayehuisha katika Uislamu… “

Yenye kutoka nje ya Shari´ah ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hayamo ndani ya Uislamu. Amesema:

“Atakayehuisha katika Uislamu mwenendo mzuri… “

Kutokana na haya tunapata kujua kwamba mwenendo huu ni lazima uwe katika yale mambo yaliyothibitishwa na Uislamu. Vinginevyo sio mwenendo wa Uislamu.

Atakayejua sababu ya Hadiyth tuliyoitaja basi atajua kuwa ´mwenendo` uliokusudiwa ni mtu kukimbilia kufanya jambo au yeye akatangulia kuitendea kazi Sunnah. Kwa msemo mwingine mtu huyo ndiye akawa wa kwanza kuitendea kazi. Kwani sababu ya Hadiyth inajulikana: kuna kundi la watu walikuja kwa Mtume  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambao walikuwa mafukara. Ndipo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawahimiza waislamu wawape swadaqah. Mtu mmoja wa Answaar akaja na mfuko wa fedha uliokuwa mzito kiasi cha kwamba ulikuwa unakaribia kumshinda kubeba na akauweka mbele yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ndipo akasema:

“Atakayehuisha katika Uislamu mwenendo mzuri basi atapata ujira wake na ujira wa atakayeutendea kazi hadi siku ya Qiyaamah.”

Kutokana na haya tumepata kujua kwamba ´kuhuisha` haina maana ya kuiweka Shari´ah. Makusudio ni yule atakayekuwa wa kwanza kuitendea kazi. Kwa sababu kwa kitendo chake anakuwa ndiye kiongozi wa watu na hivyo anakuwa ni kiigizo chema na kizuri. Matokeo yake analipwa thawabu zake na thawabu za wale wataomuigiza hadi siku ya Qiyaamah.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Manhaj Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah fiy-´Aqiydah wal-´Amal, uk. 23
  • Imechapishwa: 24/07/2019