12. Lau mambo yangelikuwa kama anavyosema padiri wa kimorocco

Moja katika utata wanaotumia wamisionari wa kikristo hii leo kwa vijana wa Kiislamu wenye kughurika uwepesi wanasema ya kwamba Allaah amewadhamini ushindi na utukufu katika sura “Aal ´Imraan”:

إِذْ قَالَ اللَّـهُ يَا عِيسَىٰ إِنِّي مُتَوَفِّيكَ وَرَافِعُكَ إِلَيَّ وَمُطَهِّرُكَ مِنَ الَّذِينَ كَفَرُوا وَجَاعِلُ الَّذِينَ اتَّبَعُوكَ فَوْقَ الَّذِينَ كَفَرُوا إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ ۖثُمَّ إِلَيَّ مَرْجِعُكُمْ فَأَحْكُمُ بَيْنَكُمْ فِيمَا كُنتُمْ فِيهِ تَخْتَلِفُونَ

“Allaah aliposema: “Ee ‘Iysaa! Hakika Mimi nitakuchukua na kukupandisha Kwangu na nitakutakasa kutokana na wale waliokufuru na nitawafanya wale waliokufuata kuwa juu ya wale waliokufuru mpaka siku ya Qiyaamah; kisha Kwangu ndio marejeo yenu nitahukumu baina yenu katika yale mliyokuwa kwayo mkikhitilafiana.” (03:55)

Kuna kijana mmoja wa Morocco alinieleza kuwa kuna padiri mmoja wa Morocco aliyeko Rabat ambaye alikipamba chumba kwa samani ambapo vijana wa kimorocco wanaishi bure ili kuwavuta kwake na kuitia dini yao katika majaribio. Padiri yule akawaambia:

“Mkiwaona wakristo ni wenye nguvu, matajiri, wenye furaha na washindi ulimwenguni msishangae. Kwani Qur-aan imewaahidi hilo.”

Kisha akawatajia Aya iliyotangulia. Wakamuamini. Hakuna yeyote aliyekuwa akijua maana halisi ya Aya. Nikamwambia kijana yule:

“Amekudanganyeni na kukuhadaeni. Mambo yangelikuwa kama anavyosema basi wangelishinda wakristo wa Najraan. Walikuwa na wapiganaji 120.000 lakini wakafanya mkataba wa amani na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kulipa kodi.

Lau mambo yangelikuwa kama anavyosema basi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) asingelishinda katika vita vya Tabuuk na kuwashtua warumi ambao walikuwa wakiogopa kumpiga vita.

Lau mambo yangelikuwa kama anavyosema basi warumi wa kibyzantine wasingelishindwa Shaam ambayo ndio Syria ya leo. Waliiacha baada ya kuhukumu kwa muda mrefu.

Mambo yangelikuwa kama anavyosema basi Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wasingeliwashinda wakristo wa Misri.

Mambo yangelikuwa kama anavyosema basi waafrika wa magharibi wasingeishinda Hispania na kusini mwa Ufaransa na Hispania ikazihukumu pamoja na waarabu kwa miaka 800.

Mambo yangelikuwa kama anavyosema basi wakristo wasingelishindwa katika vita vya Constantinople vilivyoshinda waislamu. Mpaka hii leo mji huo uko mikononi mwa waislamu.

Aya inawahusu waislamu wanaomuabudu Allaah peke yake na wanawaamini Mitume wote wa Allaah na vitabu Vyake. Makafiri wanaokusudiwa katika Aya ni wale wasiomuamini Allaah, wasiomuabudu Yeye peke yake au wanakanusha baadhi ya vitabu au Mitume.

Aya ni hoja kwa waislamu wa leo, na sio kwa maadui wao.”

Kijana yule akashangaa. Yote haya yalikuwa hayajulikani kwake, lakini hivi sasa yote yemekuwa wazi. Waislamu wengi leo ni kama shairi linavyosema:

Wenye kutusi wanadai kuwa niko katika uzito

Wamesema kweli lakini uzito wangu haujaisha

Jambo la kushangaza ni kuwa wakristo pindi wanapoisoma Qur-aan basi hawafanyi hivo kwa ajili ya kutafuta haki, bali wanafanya hivo kwa ajili ya kutafuta kasoro. Kwa mfano wanauliza:

“Muhammad amekitoa wapi kisa hiki?”

Hawaachi kuendelea kuchimba. Wanapopata kisa chenye kufanana katika Taurati, Injili au Talmud hufurahi sana kabisa, wanadhani kuwa wamepata kitu kilichokuwa kimepotea na kudai kuwa kisa hicho wao ndio wako na msingi wake. Wala hawajali zile tofauti nyingi zilizoko kwenye visa vyote viwili au kwenye Shari´ah zote mbili.

  • Mhusika: ´Allaamah Muhammad Taqiyy-ud-Diyn al-Hilaaliy al-Maghribiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Baraahiyn al-Injiylyyah ´alaa anna ´Iysaa daakhil fiyl-´Ubuudiyyah wa la hadhdhwa lahu fiyl-Uluuhiyyah, uk. 31-32
  • Imechapishwa: 16/10/2016