Ya nne: Jaabir amepokea tena:

“Kwamba baba yake alikufa shahidi siku ya Uhud na ameacha wasichana sita na ameacha deni [Wasq thelathini]. [Wadeni wakawa wakali kwa haki zao]. Alipofikiwa na kipindi cha kuvuna tende, nilimjia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) nikasema: “Ee Mtume wa Allaah! Hakika umejua kuwa baba yangu aliuwawa shahidi siku ya Uhud na ameacha madeni mengi. Mimi napenda wale wadeni wakuone wewe.” Akasema: “Nenda na uweke kila aina ya tende peke yake.” nikafanya hivo. Kisha nikamwita [akatuamkia asubuhi mapema]. Walipomuona muda ule wakaniita kwa sauti ya juu na huku wakisisitiza. Alipoona kile wanachokifanya akazunguka katika rundo kubwa zaidi kuliko marundo yote yale mara tatu [na akaliombea baraka] kisha akakaa juu yake na kusema:

“Niitikie wadeni hao. Aliendelea kuwapimia mpaka pale Allaah alipotimiza amana ya baba yangu[1] na mimi ninaapa kwa Allaah kwamba nilikuwa radhi Allaah kutimiza amana aliyoniachia baba yangu na nisirudi kwa dada zangu nikiwa na tende hata moja. Ninaapa kwa Allaah nikatoa aina zote zile kiasi cha kwamba nikawa naangalia ile aina ya tende aliyokuwa nayo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kama kwamba haijapungua tende hata moja. [Nikaenda pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuswali Maghrib na nikamweleza jambo hilo ambapo akacheka. Akasema: “Nenda kwa Abu Bakr na ´Umar na uwakhabarishe. Wakasema: “Hakika sisi tulijua pindi Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipofanya kile alichofanya kwamba yatatokea hayo.”

Ameipokea al-Bukhaariy (05/46, 171, 319, 06/462,463) mtiririko na ziada ni zake, Abu Daawuud amepokea mfano wake (02/15), an-Nasaa´iy (02/127,128), ad-Daarimiy (01/22-25), Ibn Maajah (02/82-83), al-Bayhaqiy (06/64), Ahmad (03/313, 365, 373, 391, 397) kwa kirefu na kwa kifupi.

Kwa Ahmad kuna ziada nyingi ambazo sikuzitaja kwa kuchelea kurefusha.

Ya tano: Jaabir amepokea tena akisimulia:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akitoa Khutbah kwa kusimama, akimhimidi Allaah, akimsifu kwa yale anayostahiki na akisema: “Yule aliyeongozwa na Allaah, basi hakuna wa kumpoteza, na yule aliyepotezwa na Allaah, hakuna wa kumwongoza. Hakika mazungumzo bora ni Kitabu cha Allaah, uongofu bora ni wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), uovu wa mambo ni yale yaliyozuliwa, kila kilichozuliwa ni Bid´ah [na kila Bid´ah ni upotevu na kila upotevu ni Motoni]. Macho yake yalikuwa yakipiga wekundi pindi anapotaja Qiyaamah, sauti yake inapanda juu na ghadhabu zinakuwa kali kana kwamba ni jemedari wa jeshi akisema: “Watakuvamieni asubuhi na jioni. Yeyote mwenye kuacha mali, basi ni ya warithi wake. Yeyote mwenye kuacha watoto au deni basi liko juu yangu na lielekezwe kwangu. Hakika mimi ni nina haki zaidi kwa waumini [katika upokezi mwingine imekuja: “kwa kila muumini kuliko nafsi yake mwenyewe].

Ameipokea Muslim (03/11), an-Nasaa´iy (01/234), al-Bayhaqiy katika “as-Sunan” (03/213-214) na katika “al-Asmaa´ was-Swiffaat”, uk. 82, Ahmad (03/296, 311, 338-371) na mtiririko ni wake, Abu Nu´aym katika “al-Hilyah” (03/189) na ziada ya kwanza ni yake, an-Nasaa´iy na al-Bayhaqiy na cheni ya wapokezi ni Swahiyh juu ya sharti za Muslim. Ziada ya pili ni yake na ya al-Bayhaqiy. Ya pili na ya nne ni ya Ahmad na upokezi wa pili ni wa Muslim.

Katika maudhui haya zipo Hadiyth ziliozopokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah kwa al-Bukhaariy na Muslim na wengineo[2].

Ya sita: ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote atakayebeba kutoka katika Ummah wangu deni kisha akafanya bidii kulilipa ambapo akafa bila kulilipa, basi mimi ndiye walii wake.”

Ameipokea Ahmad (06/74) kwa cheni ya wapokezi Swahiyh juu ya sharti za al-Bukhaariy na Muslim. al-Mundhiriy amesema (03/33):

“Ameipokea Ahmad kwa cheni nzuri, Abu Ya´laa, at-Twabaraaniy katika “al-Awsatw” na mfano wake katika “al-Majma´” (04/132) isipokuwa amesema:

“Wapokezi wa Ahmad ni wapokezi Swahiyh.”

Katika “al-Fath al-Baariy” (05/54) kuna faida muhimu juu ya masuala haya.

[1] Wasia wake kwangu kuhusu kulipa madeni yake.

[2] Halafu nikakusanya njia za Hadiyth hii na mapokezi yake katika juzu la kujitegemea kwa jina “Kutwbat-ul-Haajah”. Kimechapishwa.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 28-30
  • Imechapishwa: 30/12/2019