12. Kuchelewesha swalah ya Fajr ni dhambi kubwa


Swali 12: Kuna mtu anadhibiti swalah isipokuwa swalah ya Fajr ambayo huiswali pale anapoamka kutoka usingizini na haiswali msikitini. Je, inafaa kufanya hivo[1]?

Jibu: Janga hili wametumbukia watu wengi ndani yake. Watu wengi wanakesha usiku kwenye TV au katika mambo mengine. Inapofika Fajr wanakuwa wamelala na hawaamki kuswali. Hii ni dhambi kubwa. Haijuzu kwa muislamu kuifanya. Mtu akikusudia kufanya hivo basi yuko katika khatari kubwa. Kwani baadhi ya wanazuoni wameonelea kuwa ni kafiri akikusudia kuiacha ikatoka nje ya wakati wake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema katika Hadiyth Swahiyh:

“Ahadi iliopo kati yetu sisi na wao ni swalah. Hivyo basi, yule atakayeiacha amekufuru.”[2]

Ameipokea watunzi wa Sunan kwa cheni ya wapokezi Swahiyh.

Amesema tena (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Baina ya mtu na shirki na ukafiri ni kuacha swalah.”[3]

Ameipokea Muslim.

Kwa hivyo ni lazima kwa mtu huyu na wale wengine ambao wanakesha wamche Allaah na wapupie kulala mapema ili waweze kuswali pamoja na watu swalah ya Fajr. Kuhusu ambaye anaiswali baada ya kuchomoza jua wakati anapoamka kwa ajili ya kazi yake ya kidunia, hii ni dhambi kubwa ambayo anastahiki kutiwa adabu na kupewa adhabu mbaya. Akitubia, ni sawa, na vinginevyo auliwe kutokana na kitendo hichi.

Ni wajibu kwa watawala kumtaka atubie. Akitubia, ni sawa, na vyenginevyo auliwe hali ya kuwa kafiri au adhabu juu ya ile tofauti walionayo wanazuoni.

Kwa kumalizia ni kwamba hii ni dhambi kubwa waliyopewa kwayo mtihani watu wengi. Sababu yake ni kukesha na kuchukulia wepesi wa kutolala mapema. Unapofika wakati wa swalah wanakuwa kama wafu wasioweza kuamka, jambo ambalo sio udhuru kwao. Ni lazima kwao kumcha Allaah, waharakie kulala na watafute msaada kwa masaa ambayo wanasikia sauti zake wakati wa adhaana ya Fajr au kuwaamsha kutoka katika jamaa zao au wengineo kisha waswali pamoja na wengine. Haifai kwao kuswali majumbani au kuswali baada ya kuchomoza kwa jua. Yote haya ni haramu na ni dhambi ambayo haitakikani kuinyamazia. Bali ni lazima kwao kuswali ndani ya wakati na waswali pamoja na waislamu katika misikiti. Haifai kwao kuchelewesha ambapo wakaswali majumbani ijapo ni ndani ya wakati. Kama ambavo pia haifai kwao kuichelewesha mpaka baada ya kuchomoza kwa jua, jambo ambalo ni khatari na baya zaidi.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (12/69-71).

[2] Ahmad (21859) na at-Tirmidhiy (2545).

[3] Muslim (82).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam Swalaat-il-Jumu´ah wal-Jamaa´ah, uk. 37-38
  • Imechapishwa: 26/11/2021