12. Jambo la kwanza linalofunguza: Kula na kunywa kwa kukusudia

Suala la pili: Mambo yanayomfunguza mfungaji

Ni yale mambo ambayo yanayomuharibia mfungaji swawm yake na yakamfunguza. Mfungaji anakuwa ni mwenye kufungua kwa kufanya moja katika vitu vifuatavyo:

1- Kula au kunywa kwa kukusudia. Amesema (Ta´ala):

وَكُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الْأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِ ۖ ثُمَّ أَتِمُّوا الصِّيَامَ إِلَى اللَّيْلِ

“Kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu uzi mweupe wa alfajiri kutokana na uzi mweusi Kisha timizeni funga mpaka usiku.”[1]

Aayah imebainisha kwamba haijuzu kula na kunywa baada ya kuchomoza kwa alfajiri mpaka uingie usiku ambapo ni kuzama kwa jua. Lakini kwa yule mwenye kula au kunywa kwa kusahau swawm yake ni sahhi. Ni lazima kwake kujizuia atapokumbuka au akakumbushwa kuwa amefunga. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mwenye kusahau ilihali amefunga ambapo akala au akanywa, basi aikamilishe funga yake. Hakika si vyenginevyo Allaah ndiye kamlisha na kumpa maji.”[2]

Pia swawm inaharibika kwa kupitisha dawa kupitia njia ya pua na kwa kila kinachofika kooni, ijapo si kwa njia ya mdomo, katika vile vitu vyenye hukumu ya kula na kunywa. Kama mfano wa sindano za lishe.

[1] 02:187

[2] al-Bukhaariy (1933) na Muslim (1155).

  • Mhusika: Nukhbatin minal-´Ulamaa´
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fiqh-ul-Muyassar, uk. 157
  • Imechapishwa: 23/04/2020