Ndugu wapendwa! Anaweza kusema mwenye kusema: Kwa nini mnatilia nguvu nyingi kwa Suufiyyah na kumnukuu Ibn ´Arabiy, Ibn-ul-Faaridhw na wengineo ambao wameshakufa miaka mia kadhaa iliyopita? Ingelikuwa bora kuwaradddi wakomunisti, wakanamungu na wale ambao wanahukumu kwa kanuni na wanaacha kuhukumu kwa Shari´ah ya Allaah. Kwa nini msiraddi mapote potevu kama Qaadiyaaniyyah, Bahaaiyyah na Nuswayriyyah? Najibu kwa kusema:

Ni wajibu kwa kila Muislamu, khaswakhaswa wanafunzi na wale wanaolingania katika Uislamu, kutumia juhudi kubwa kupiga vita mambo yote yanayoenda kinyume na Shari´ah ya Uislamu, sawa ikiwa inahusiana na wakomunisti, wakanamungu, waabudia makaburi na Suufiyyuun. Nimeona walinganizi wengi ambao wamefanyia hilo juhudi, ambao tayari wamejishughulisha kwa kutilia umuhimu baadhi ya sehemu yake, lakini wameacha sehemu nyingine. Bali yaonekana kana kwamba wamelisahau suala hili, kwa sababu tunaona ni wachache wenye kutilia umuhimu kutahadharisha upotevu na uzushi wa Suufiyyuun. Huenda baadhi ya watu wakawakasirikia wale ambao wanawaita katika kusahihisha ´Aqiydah na kutahadharisha Suufiyyah na wale ambao wanawaomba mawalii, kwa hoja eti kitendo hicho kinawagawanya Waislamu. Bali tumeona baadhi ya walinganizi maarufu wakihuisha ulinganizi wa kuwafuata Suufiyyah na wakitunga vitabu juu ya hilo kama mfano wa kitabu kwa jina “Tarbiyatanaa ar-Ruuhiyyah” au “Taswawwuf al-Harakat-ul-Islaamiyyah”[1].

Ndani ya kitabu hiki anaweka wazi mapenzi yake kwa Suufiyyah na kuamini kwake uongo wao na “makarama yao”. Msikilize anavyosema wakati alipokuwa anaelezea “makarama” ya Suufiyyah na khaswa kuhusu Twariyqah ar-Rafaa´iyyah. Anasema katika ukurasa wa 217:

“Kukanusha msingi wa makarama inayopitika kati ya Suufiyyah, ni ukanushaji wa pasi na ujuzi na wa kimakosa. Mambo muhimu kabisa ambayo yanakanushwa ni yale yanayopitika kwa Twariyqah ar-Rafaa´iyyah, si moto, risasi wala panga haviwaathiri. Haya ni matendo ambayo yameenea na yanayojulikana yaliyoshuhudiwa. Wengi katika wale ambao walikuwa wanayapinga, huyafanyia utafiti na kujirudi katika kupinga kwao. Yale yanayoshuhudiwa kwao haiwezekani ikawa ni uchawi, kwa kuwa uchawi uko katika ulimwengu ambapo sababu na njia zinapokuja na hautumiwi hapa. Kama jinsi hauwezi kuwa kwa njia ya mazoezi ya kiroho, kwa kuwa hili linawapitikia hata wale ambao hawakufanya mazoezi ya kiroho. Hili linapitika kwa sababu amekula kiapo cha usikivu kutoka kwa Shaykh. Bali wakati mwingine linaweza kumpitikia yule ambaye hakula kiapo. Siku moja kuna mkristo alinieleza kuhusu tukio lililompitikia yeye, ni tukio linalojulikana. Baada ya kusikia kinasemwa kutoka kwa mtu mwingine, Allaah Akanikutanisha na mtu huyo. Akanieleza kwamba alihudhuria halaka ya Dhikr. Akaja mmoja katika waliokuwa pale na kumdunga msumari mgongoni na ukatokezea kifua mwake na akaushika. Kisha akausukuma tena na haukuacha athari yoyote wala donda.”

Mwandishi anachukua umakini wa kuraddi hoja za anayesema kwamba matukio haya yanampitikia mtenda madhambi tu na si mcha Mungu, vipi matukio haya ya makarama yanaweza kumpitikia mtu ambaye sio mcha Mungu? Anasema:

“Hoja kubwa za wale wanaopinga haya, ni kwamba mambo haya yasiyokuwa ya kawaida yanawapitikia watenda madhambi na kadhalika kwa watu wema, jambo ambalo ni kweli. Lakini sababu ya hilo ni kwamba makarama sio yao, bali asli ni ya Shaykh ambaye Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) Amempa karama hizi na Akaifanya kuwa ni yenye kupitika kati ya wafuasi wake.”

Hii sio ajabu kuona mtu mjuzi akadanganywa na michezo hii ya ki-Shaytwaan na akaisadikisha, kwa vile anazingatiwa kuwa ni mmoja katika viongozi wao wakuu? Anakubaliana ya kwamba makarama ya Suufiyyah ni ya kihakika na kwa ajili hiyo haitakikani kwa yeyote kuyakanusha. Sisi tunamwambia yale ambayo yatamzuia kuchukua uchawi au baadhi ya njia zingine za udanganyifu, kama alivyosema Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) wakati alipowapa changamoto baadhi ya wafuasi wa Twuruq as-Suufiyyah. Kwa uongo wanadai kwamba wanaweza kupita juu ya moto kwa usalama kabisa. Hivyo akasema kuwaambia waoshe kwanza miili yao kwa siki na maji ya moto kabla ya kuanza kupita juu ya moto. Wakakataa na kuogopa. Hili ni kutokana na kwamba alifichua udanganyifu wao ambao walikuwa wakitumia. Walikuwa wakipaka miili yao mafuta ya chura, maganda ya machungwa makali, unga wa madini na vinginevyo katika udanganyifu waliokuwa wakijulikana nao. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

“Yanaweza pia kufanywa kwa msaada wa Mashaytwaan wao, kwa sababu ni watu ambao wako karibu na Mashaytwaan kama jinsi wao walivo kwa ndugu zao. Pindi wanapojiunga ili kupiga filimbi na kupiga makofi, huzidiwa na hali ambayo hupiga makelele na kucheza kama waliopatwa na mapepo pamoja na kuzungumza kwa lugha ambayo hawaifahamu wao wala wale waliohudhuria. Ni Mashaytwaan wao ndio huzumgumza kwa ndimi zao wakati wanapopotewa na akili zao kama jinsi jini linavyozungumza kwa ndimi ya liliyemsibu. Ikiwa mtu yuko na jamaa aliyesibiwa, anawapa kitu ili kuweza kuja. Halafu wanapiga ngoma na ala zingine za muziki na hukonga moto mkubwa. Kisha wanaweka chuma kikubwa kwenye moto huo na kuchomeka mikuki yenye ncha za chuma. Baada ya hapo mmoja wao anapanda juu na kukaa kwenye mikuki hii mbele za watu. Kisha anachukua chuma hicho cha moto na kukiingiza kwenye mkono wake na mfano wa hayo. Watu wanaona mawe yanaruka bila kumuona yule mwenye kuyarusha. Yote haya yanatoka kwa wale Shaytwaan, ambao wana mawasiliano ya moja kwa moja na moto, ambao huwasaidia juu ya mikuki hii. Inaweza kuwa vilevile kwamba wale watu walioshiriki wasiweze kuhisi kitu, kama jinsi yule aliyesibiwa (aliye uwanjani) hahisi kitu pindi anapopata kipigo, kwa kuwa kipigo hicho kinawapata majini. Namna hiyo ndivyo inavyokuwa hali ya wale wanaoshiriki katika matokeo ya ki-Shaytwaan. Kwa ajili hiyo, kadri jinsi mtu anavyokuwa ni mwenye kufanana na majini na Mashaytwaan katika matendo yao, ndivyo jinsi hali yake inakuwa na nguvu zaidi. Vilevile hali hii huwa katika sehemu za wito wa ki-Shaytwaan na kisomo chake. Mizumari na ala za muziki ndio wito wake na nyimbo ndio kisomo chake. Haya hayatoki kabisa kwa wale wanaoswali, wanaomdhukuru Allaah, wanaomba Du´aa na Qur-aan inaposomwa. Matendo haya wanayofanya, hayana faida katika Uislamu wala dunia. Watu hawa ambao wana hali kama hizi za ki-Shaytwaan wanajikuta wako katika utatizi. Kutokana na ugugu wao wanaondoshewa baraka zote. Wanachozidishiwa tu ni khofu. Kutokana na kutokuwa kwao na ucha Mungu wanakula mali za watu kwa batili na hawaamrishi mema, kukataza maovu na wala hawapigani Jihaad katika njia ya Allaah.”[2]

Ndugu watukufu! Kujigamba kuwa na makarama sio katika alama za watu wema katika Maswahabah, waliokuja baada yao, maimamu wa Waislamu wala wanachuoni wa Waislamu baada yao. Hatukusikia kukitajwa kitu kutoka kwa Swahabah yeyote, waliokuja baada yao wala maimamu wane Maalik, Abu Haniyfah, ash-Shaafi´iy wala Ibn Hanbal (Rahimahumu Allaah). Hatukusikia kutoka kwa yeyote kwamba alipitikiwa na kitu mfano wa hayo. Wala hakuna yeyote katika wao aliyeingia kwenye moto au kujipiga msumari au upanga kisha akawa hai tena. Kadhalika haya hayakufanywa wala na wanachuoni wakubwa wa leo, kama kwa mfano wa Shaykh ´Abdul-´Aziyz bin Baaz na Shaykh ´Abdullaah bin Humayd. Matendo haya yanaweza kupatikana tu kati ya Suufiyyah – tokea zamani mpaka hii leo. Bila ya shaka hii ni dalili tosha kubwa kuonyesha kuwa ni matendo ya ki-Shaytwaan na wala sio makarama kutoka kwa Mwingi wa Rahmah.

Ninarudi nilipoanzia na kusema. Kutokana na nilivyoona walinganizi wengi wamepuuza vipengele muhimu vya Uislamu – navyo ni kulingania katika kumpwekesha Allaah na kuzisahihisha ´Aqiydah kutokana na shirki, jambo ambalo linahusiana na kuwaabudia mawalii, kukaa kwa muda mrefu kwenye makaburi yao, kuwaomba wafu na viumbe visivyoonekana – na wananyamazia upotevu mwingine unaofanywa na Twuruq as-Suufiyyah waliopo leo – jambo ambalo limeenea sana katika miji ya Kiislamu, na yule atayetoka nje ya nchi hii (yaani Saudi Arabia), ataona nguvu ambazo Suufiyyuum walizonazo kati ya Waislamu Misri, Syria, Marocco, Afrika, India na kwenginepo, sawa ikiwa inahusiana na Rifaa´iyyah, Tijaaniyyah, Ahmadiyyah, Qaadiriyyah, Burhaamiyyah, Shaadhiliyyah, Khattwaaniyyah, Darqaawiyyah au Naqshbandiyyah – ndio nikapenda kukumbusha na kuzindua kitu ambacho naamini kuwa ni muhimu sana. Kadhalika napendelea kuwapa ndugu zangu, ambao wanasoma Daar-ul-Haadiyth tukufu na wenye kutoka nchi mbalimbali za Kiislamu ambapo kunapatikana Twuruq as-Suufiyyah nyingi, sehemu ya elimu na kinga dhidi ya maradhi ya Suufiyyah yenye kuangamiza. Kama jinsi yanapatikana maradhi yanayoupata mwili, kuna maradhi pia yanayozipata roho na nyoyo. Kwa hivyo ndio maana inatakikana kwa wanachuoni na walinganizi kutilia umuhimu kuzipa nyoyo kinga, kama jinsi madaktari wanavyotilia umuhimu kuipa kinga miili.

Swalah na salamu zimwendee Muhammad, familia yake na Maswahabah zake.

[1] Malezi yetu ya kiroho au hakarati za Kiislamu za Suufiyyah. Imeandikwa na Sa´iyd Hawaa.

[2] Majmuu´-ul-Fataawaa (11/495-496.

  • Mhusika: Shaykh Muhammad bin Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Haqiyqat-us-Suufiyyah
  • Imechapishwa: 25/12/2019