Hadiyth ya saba

7- ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema.

“Mwenye kufa na juu yake yuko na swawm basi afungiwe na walii wake.”

Ameipokea Abu Daawuud na akasema: “Hili linahusu katika nadhiri tu. Vilevile ndio maoni ya Ahmad bin Hanbal.”

Maana ya kijumla:

Madeni yaliyoko kwa maiti ni lazima kuyalipa. Ni mamoja yakawa ni haki ya Allaah, kama vile zakaah na swawm, au ni haki ya wanaadamu, kama vile madeni ya kimali. Bora jambo hilo likasimamiwa na warithi wake. Ndio (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Mwenye kufa na juu yake yuko na swawm basi afungiwe na walii wake.”

Faida zinazochukuliwa kutoka katika Hadiyth:

1- Udhahiri wa Hadiyth ni kwamba ni wajibu kumlipia maiti swawm. Ni mamoja ikawa ni nadhiri au ni wajibu kimsingi wa Shari´ah. Tofauti na Abu Daawuud alivoliwekea hilo mpaka.

2- Ambaye atasimamia jambo hilo ni walii wake. Makusudio ni warithi wake ambao watanufaika baada ya kufa kwake. Muqtadha wa kumtekelezea wajibu wake ni kumlipia deni alilonalo kwa Allaah.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdullaah bin ´Abdir-Rahmaan al-Bassaam
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Taysiyr-ul-´Allaam Sharh ´Umdat-il-Ahkaam, uk. (01/332-333)
  • Imechapishwa: 08/06/2018