12. Hadiyth “Mtu yeyote ambaye atasimama kwa ajili ya kutawadha… “

187 – Abu Umaamah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mtu yeyote ambaye atasimama kwa ajili ya kutawadha hali ya kuwa amelenga swalah kisha akaosha viganja vyake vya mikono, basi hudondoka kila kosa katika kiganja vya mkono wake kwa lile tone la kwanza tu. Akisukutua, akapalizia na kupenga, basi hudondoka makosa kutoka katika ulimi na midomo yake kwa lile tone la kwanza tu. Akiosha uso wake, basi hudondoka kila kosa kutoka katika usikizi na uoni wake kwa lile tone la kwanza tu. Akiosha mikono yake mpaka katika visugudi, na miguu yake mpaka kwenye vifundo vya miguu, basi husalimika na kila dhambi kama alivokuwa ile siku aliyozaliwa na mama yake. Akisimama kwa ajili ya kuswali, basi Allaah hunyanyua ngazi yake, na kama ataketi chini basi anaketi chini hali ya kuwa amesalimika.”[1]

Ameipokea Ahmad na wengineo kupitia kwa ´Abdul-Hamiyd bin Bahraam, kutoka kwa Shahr bin Hawshab. at-Tirmidhiy ameifanya kuwa nzuri kupitia zengine. Cheni ya wapokezi wake ni nzuri kutokana na nyenginezo; haina neno. Ameipokea vilevile kupitia njia ambayo ni Swahiyh na amezidisha juu yake kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Wudhuu´ unafuta yale ya kabla yake ambapo ile swalah inakuwa ni ziada ya thawabu.”[2]

Katika tamko jengine amesema Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Akitawadha mtu muislamu, basi zinaondoka dhambi kutoka kwenye usikizi, uoni, mikono na miguu yake. Akiketi chini, basi huketi hali ya kuwa amesamehewa.”[3]

 Cheni ya wapokezi ni nzuri.

Katika tamko lake jengine imekuja:

“Muislamu akitawadha ambapo akaosha miguu yake, basi husamehewa yale yaliyofanywa na mikono yake. Akiosha uso wake, basi husamehewa yale yaliyotazamwa na macho yake. Akipangusa kichwa kwa mikono yake, basi husamehewa yale yaliyosikiwa na masikio yake. Akiosha miguu yake, basi husamehewa yale yaliyoendewa na miguu yake. Kisha anasimama kwa ajili ya kuswali ambapo hulipwa zaidi.”[4]

Cheni ya wapokezi ni nzuri.

Katika upokezi mwingine wa at-Twabaraaniy katika “al-Mu´jam al-Kabiyr” unasema inafuatavyo:

“Abu Umaamah amesema: “Lau nisingeyasikia haya kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiyasema mara saba, basi nisingeyasimulia: “Akitawadha mtu kama alivoamrishwa, basi huondoka madhambi kutoka kwenye usikizi, uoni, mikono na miguu yake.”

 Cheni ya wapokezi ni nzuri.

[1] Swahiyh kupitia zengine.

[2] Swahiyh kupitia zengine.

[3] Swahiyh kupitia zengine.

[4] Swahiyh kupitia zengine.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Adhwiym bin ´Abdil-Qawiy al-Mundhiriy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb (1/192-194)
  • Imechapishwa: 14/04/2021
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy