Ni wajibu kwa muumini kuamini kuwa Qadar yote imepangwa na Allaah (Tabaarak wa Ta´ala); kheri na shari yake. Miongoni mwa watu ikiwa ni pamoja na Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) katika “al-Waasitwiyyah” ametaja kuwa Qadar ina daraja nne:

Daraja ya kwanza: Allaah anajua kila kitu. Allaah kwa elimu Yake ya milele daima ana ujuzi juu ya viumbe Vyake; vikubwa na vidogo, visivyoonekana na vyenye kuonekana.

Kisha baada ya hapo akayaandika yote kwenye Ubao uliohifadhiwa. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah amepanga makadirio ya viumbe miaka elfu khamsini kabla ya Kuumba mbingu na ´Arshi Yake ilikuwa juu ya maji.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema tena:

“Kitu cha kwanza alichoumba Allaah ilikuwa ni kalamu. Akaiambia: “Andika.” Ikasema: “Ee Allaah! Niandike nini?” Akasema: “Andika makadirio ya kila kitu mpaka siku ya Qiyaamah.”[2]

Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) akaandika kwenye Ubao uliohifadhiwa yale yote anayoyajua kwa ujuzi wake ulioenea:

وَعِندَهُ مَفَاتِحُ الْغَيْبِ لَا يَعْلَمُهَا إِلَّا هُوَ ۚ وَيَعْلَمُ مَا فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ ۚوَمَا تَسْقُطُ مِن وَرَقَةٍ إِلَّا يَعْلَمُهَا وَلَا حَبَّةٍ فِي ظُلُمَاتِ الْأَرْضِ وَلَا رَطْبٍ وَلَا يَابِسٍ إِلَّا فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ

“Na Kwake zipo funguo za mambo yaliyofichikana; hakuna azijuaye isipokuwa Yeye tu. Anajua yale yote yaliyomo nchikavu na baharini; halianguki jani lolote ila Hulijua na wala punje katika viza vya ardhi na wala kilichorutubika na wala kikavu isipokuwa kimo katika Kitabu kinachobainisha wazi.”[3]

يَا بُنَيَّ إِنَّهَا إِن تَكُ مِثْقَالَ حَبَّةٍ مِّنْ خَرْدَلٍ فَتَكُن فِي صَخْرَةٍ أَوْ فِي السَّمَاوَاتِ أَوْ فِي الْأَرْضِ يَأْتِ بِهَا اللَّـهُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ لَطِيفٌ خَبِيرٌ

“Ee mwanangu! Hakika likiweko lolote [ulilofanya] lenye uzito wa punje ya hardali likawa katika jabali au mbinguni au ardhini, basi Allaah atalileta tu. Hakika Allaah ni Mwenye kuyaendesha mambo kwa ulatifu, Mwenye khabari juu ya kila kitu.”[4]

Allaah ameyajua mambo yote na ameyaandika kwenye Ubao uliohifadhiwa.

Daraja ya pili: Utashi wa Allaah ulioenea kila kitu na kila kinachopatikana kimepatikanaka kwa sababu Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ametaka hivo.

Halafu inatakiwa kuamini uwezo wa Allaah ambao kwa uwezo huo anaumba kila kitu. Hakuna kitu kisichopatikana au kinachopatikana, kidogo au kikubwa, neno au tendo, harakati au utulivu, isipokuwa Allaah ametaka iwe hivo. Hakuna kitu katika hivyo vilivyotajwa isipokuwa Allaah amekiumba kwa kutaka Kwake na kwa uwezo Wake usioshindwa na kitu.

Pamoja na hivyo Allaah ametuma Mitume na akateremsha Vitabu ambavyo amewaamrisha waja maamrisho, makatazo, I´tiqaad, ´ibaadah na kadhalika. Mwenye kutii anatii kwa sababu Allaah anataka hivyo pasi na hilo kupingana na utashi na uwezo wa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Mwenye kutii na akawafuata Mitume watukufu malipo yake ni Pepo. Yule mwenye kuwaasi na akawakadhibisha anaadhibiwa kutokana na upindaji wake. Ikiwa upindaji wake unahusiana na kufuru, anatumbukia na kudumishwa Motoni milele, na ikiwa inahusiana na madhambi makubwa, ni jambo la khiyari kwa Allaah akitaka atamsamehe na akitaka atamuadhibu.

[1] Muslim (2653).

[2] Abu Daawuud (4700).

[3] 06:59

[4] 31:16

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 374-375
  • Imechapishwa: 30/07/2017