12. Dalili ya tatu kwamba yule asiyeswali sio kafiri

Fungu la tatu: Dalili za jumla zilizofungamana kwa njia ya kwamba hakuwezi kuhusiana na kuacha swalah. Mfano wa dalili hizo ni maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Allaah amemharamishia Moto yule mwenye kusema hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah akikusudia kwa kufanya hivo uso wa Allaah.”[1]

“Hakuna yeyote atayeshuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, akiwa ni mkweli kutoka kwenye moyo wake, isipokuwa Allaah atamharamishia Moto.”

Kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume Wake kumefungamanishwa na kufanya hivo kwa moyo wa ukweli. Hakuna mtu mwenye kuitamka kikweli akaacha swalah. Kwani swalah ndio nguzo ya Uislamu na ndio uhusiano baina ya mja na Mola Wake. Akiwa ni mkweli kabisa na anatafuta uso wa Allaah basi atayafanya yale yenye kumfikisha huko na kujiepusha na yale yenye kumzuia kufika huko. Ambaye anashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah akiwa ni mkweli moyoni mwake basi ni lazima ukweli huo umfanye kutekeleza swalah hali ya kumtakasia Allaah nia na kuitekeleza kama alivyoitekeleza Mtume wa Allaah (Swalla Allahu ´alayhi wa sallam). Hayo ndio yanayopelekewa na shahaadah ya kikweli.

[1] al-Bukhaariy (425) na Muslim (33).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Hukm Taarik-is-Swalaah, uk. 14-15
  • Marejeo: Firqatunnajia.com
  • Imechapishwa: 22/10/2016