12. Dalili ya kumi kutoka katika Sunnah kwamba Allaah yuko juu ya viumbe

10- ´Abdullaah bin Muhammad ametukhabarisha: ´Abdul-Qaadir bin Muhammad ametuhadithia: al-Hasan bin ´Aliy ametuhadithia: Ahmad bin Ja´far ametuhadithia: ´Abdullaah ametuhadithia: Baba yangu ametuhadithia: Husayn bin Muhammad ametuhadithia: Ibn Abiy Dhi’b ametuhadithia, kutoka kwa Muhammad bin ´Amr bin ´Atwaa’, kutoka kwa Sa´iyd bin Yasaar, kutoka kwa Abu Hurayrah, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyesema:

“Wakati mtu anapokufa ikiwa mtu alikuwa mwema anajiwa na Malaika ambao wanasema: “Toka, ee nafsi nzuri iliokuwa kwenye mwili mzuri. Toka ukiwa ni mwenye kusifiwa na pata bishara njema ya rehema, mimea yenye harufu nzuri na Mola si Mwenye kukasirika.”Kutaendelea kusemwa hivo mpaka pale inapotoka. Halafu ipandishwe juu mbinguni. Itaombewa idhini ya kuingia ambapo kutasemwa: “Ni nani huyu?”Kutasemwa kwamba ni fulani ambapo watasema: “Karibu, ee nafsi nzuri iliokuwa kwenye mwili mzuri. Ingia ukiwa ni mwenye kusifiwa na pata bishara njema ya rehema, mimea yenye harufu nzuri na Mola si Mwenye kukasirika.”Hakutoacha kuendelea kusemwa hivo mpaka ifike kwenye mbingu ambayo Allaah (´Azza wa Jall) Yuko juu yake. Na kama mtu alikuwa muovu watasema: “Toka, ee nafsi ovu iliokuwa kwenye mwili mbaya. . Toka ukiwa ni mwenye kusemwa vibaya na pata bishara ya maji yenye kuunguza, viza vya barafu na mfano wa hayo.” Kutaendelea kusemwa hivo mpaka pale inapotoka. Halafu ipandishwe juu mbinguni. Itaombewa idhini ya kuingia ambapo kutasemwa: “Ni nani huyu?”Kutasemwa kwamba ni fulani ambapo watasema: “Hukaribishwi, ee nafsi ovu iliokuwa kwenye mwili mbaya. Rudi hali ya kusemwa vibaya. Hakika hutofunguliwa milango ya mbinguni.” Kisha itarudishwa kutoka mbinguni mpaka ifike ndani ya kaburi.”[1]

[1] Ibn Maajah (4262) na Ahmad (2/364). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Sunan Ibn Maajah” (3456). adh-Dhahabiy amesema:

”Ameipokea Ahmad katika ”al-Musnad” na al-Haakim katika ”al-Mustadrak” ambaye amesema: ”Iko na masharti kama ya al-Bukhaariy na Muslim.” (al-´Uluww, uk. 22)

  • Mhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ithbaatu Swifat-il-´Uluww, uk. 82-84
  • Imechapishwa: 19/04/2018