Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

… bali Amewatumia Mtume…

MAELEZO

Allaah (´Azza wa Jall) ametutumia Mtume, Ummah wetu huu wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Mtume mwenye kutusomea Aayah za Mola wetu, kututakasa na kutufunza Qur-aan na Sunnah kama jinsi alivyowatuma wale waliokuwa kabla yetu. Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

وَإِن مِّنْ أُمَّةٍ إِلَّا خَلَا فِيهَا نَذِيرٌ

“Na hakuna Ummah wowote ule isipokuwa amepita humo mwonyaji.” (Faatwir 35 : 24)

Ni lazima kwa Allaah kuwatumilizia viumbe Mitume  ili hoja iweze kuwasimamia na wapate kumuabudu Allaah kwa mujibu wa yale anayoyapenda na kuyaridhia. Allaah (Tabaaraka wa Ta´ala) amesema:

إِنَّا أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ كَمَا أَوْحَيْنَا إِلَىٰ نُوحٍ وَالنَّبِيِّينَ مِن بَعْدِهِ ۚ وَأَوْحَيْنَا إِلَىٰ إِبْرَاهِيمَ وَإِسْمَاعِيلَ وَإِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ وَالْأَسْبَاطِ وَعِيسَىٰ وَأَيُّوبَ وَيُونُسَ وَهَارُونَ وَسُلَيْمَانَ ۚ وَآتَيْنَا دَاوُودَ زَبُورًا وَرُسُلًا قَدْ قَصَصْنَاهُمْ عَلَيْكَ مِن قَبْلُ وَرُسُلًا لَّمْ نَقْصُصْهُمْ عَلَيْكَ ۚ وَكَلَّمَ اللَّـهُ مُوسَىٰ تَكْلِيمًا رُّسُلًا مُّبَشِّرِينَ وَمُنذِرِينَ لِئَلَّا يَكُونَ لِلنَّاسِ عَلَى اللَّـهِ حُجَّةٌ بَعْدَ الرُّسُلِ ۚ وَكَانَ اللَّـهُ عَزِيزًا حَكِيمًا

“Hakika Tumekufunulia Wahy kama tumevyomfunulia Wahy Nuuh na Manabii baada yake na tumemfunulia Wahy Ibraahiym na Ismaa’iyl na Ishaaq na Ya’quub na vizazi na ‘Iysaa na Ayyuub na Yuunus na Haaruun na Sulaymaan, na tumempa Daawuud Zabuur. Na Mitume Tuliokwishakusimulia mikasa yao hapo kabla na Mitume wengine hatukukusimulia mikasa yao – na bila shaka Allaah alimzungumzisha Muusa maneno ya kweli – Mitume ni wabashiriaji na waonyaji ili pasikuweko kutoka kwa watu hoja yoyote juu ya Allaah baada ya kutumilizwa Mitume. Na Allaah ni Mwenye kabisa asiyeshindika, Mwenye hekima!” (an-Nisaa´ 04 : 163-165)

Hatuwezi kumwabudu Allaah kwa njia anayoiridhia isipokuwa kwa uongofu wa Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam). Kwa sababu wao ndio ambao wametubainishia yale anayopenda Allaah na kuyaridhia na yale yanayotukurubisha kwa Allaah (´Azza wa Jall). Kwa ajili hiyo ni katika hekima ya Allaah kutuma wajumbe wenye kutoa bishara njema na maonyo kwa watu. Dalili ni maneno Yake (Ta´ala):

إِنَّا أَرْسَلْنَا إِلَيْكُمْ رَسُولًا شَاهِدًا عَلَيْكُمْ كَمَا أَرْسَلْنَا إِلَىٰ فِرْعَوْنَ رَسُولًا فَعَصَىٰ فِرْعَوْنُ الرَّسُولَ فَأَخَذْنَاهُ أَخْذًا وَبِيلًا

“Hakika Sisi tumekutumieni Mtume awe shahidi juu yenu, kama tulivyotuma kwa Fir’awn Mtume. Lakini Fir’awn alimuasi huyo Mtume tukamchukuwa mchukuo wa kuangamiza.” (al-Muzzammil 73 : 15-16)

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 32
  • Imechapishwa: 18/05/2020