12. Bay´ah ya ´Aqabah


Katika mnasaba wa Hajj Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikutana na kundi la Answaar ´Aqabah. Wote walikuwa wanatoka al-Khazraj; Abuu Umaamah As´ad bin Zaraarah bin ´Uds, ´Awf bin al-Haarith bin Rifaa´ah, Raafi´ bin Maalik bin al-´Ajlaan, Qutbah bin ´Aamir bin Hadiydah, ´Uqbah bin ´Aamir bin Naabiy na Jaabir bin ´Abdillaah bin Ri-aab. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawalingania katika Uislamu ambapo wakasilimu moja kwa moja kuingia katika Uislamu. Kisha wakarejea al-Madiynah na wakalingania katika Uislamu. Uislamu ukaanza kuenea al-Madiynah. Hakukubaki nyumba isipokuwa Uislamu uliingia ndani yake.

Mwaka uliofuata kukaja wanaume kumi na mbili kukiwa pamoja na wale sita waliotajwa isipokuwa Jaabir bin ´Abdillaah bin Ri´aab. Kwenye jopo hilo alikuwemo Mu´aadh bin al-Haarith bin Rifaa´ah (ndugu wa ´Awf bin al-Haarith bin Rifaa´ah alotangulia kutajwa) na Dhakwaan bin ´Abdi Qays bin Khaladah. Dhakwaan alikuwa akiishi Makkah mpaka alipohamia al-Madiynah. Ndio maana inasemwa kuwa alikuwa ni Muhaajir na Answaariy yote mawili. Jopo lilikuwa pia na ´Ubaadah bin as-Swaamit bin Qays na Abuu ´Abdir-Rahmaan Yaziyd bin Tha´labah. Hawa kumi na tatu walikuwa ni al-Khazraj. Wawili walikuwa ni al-Asw: Abuul-Haytham Maalik bin at-Tayyihaan na ´Uwaym bin Saa´idah. Wakampa bay´ah Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kama jinsi wanawake walivyompa bay´ah. Walikuwa bado hawajaamrishwa vita.

Wakati waliporudi al-Madiynah Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimtuma pamoja nao ´Amr bin Umm Maktuum na Musw´ab bin ´Umayr ili kuwafunza wale wenye kusilimu Qur-aan na kulingania katika dini ya Allaah (´Azza wa Jall). Walikuwa wakiishi kwa Abuu Umaamah As´ad bin Zaraarah. Musw´ab bin ´Umayr ndiye ambaye alikuwa akiwaongoza katika swalah. Siku moja yeye mwenyewe alikusanya watu arubaini ambapo watu wengi wakaingia katika Uislamu kupitia watu hao wawili. Baadhi ya watu hao ilikuwa ni Usayd bin al-Hudhayr na Sa´d bin Mu´aadh. Wakati wawili hao waliposilimu kabila nzima pia ya Banuu ´Abdil-Ashhal ikaingia katika Uislamu, wanaume kwa wanawake. Ambaye hakusilimu tu ilikuwa ni al-Usayrim, ndugu wa ´Amr bin Thaabit bin Qays. Alichelewa kuingia katika Uislamu mpaka katika vita vya Uhud. Akapigana vita na kuuawa kabla ya kuwahi kumsujudia Allaah Sujuud moja. Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipofikia na khabari hiyo akasema:

“Amefanya dogo na atalipwa sana.”[1]

Uislamu ukazidi kukua zaidi na zaidi al-Madiynah. Musw´ab akarejea Makkah. Mwaka huo waislamu wengi wa Answaar, na washirikina, wakaenda Hajj. Wakati huo Answaar walikuwa wakiongozwa na al-Baraa’ bin Ma´ruur (radhiya Allâhu ´anh).

Theluthi ya kwanza ya usiku ya ´Aqabah wanaume sabini na tatu na wanawake wawili wakaenda kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa maficho kumpa bay´ah. Walifanya hivyo ili watu wao na makafiri wa Makkah wasiwazuie yale wanayowazuia kwayo wanawake na watoto wao. Wa kwanza kumpa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) bay´ah ilikuwa ni al-Baraa’ bin Ma´ruur. Akapata utukufu wa kusaini na kuongoza makubaliano.

al-´Abbaas, ami ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), akahudhuria wakati wa bay´ah ili kuihakikisha. Pamoja na kuwa alikuwa bado yuko katika dini ya mababu zake. Usiku huo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akateua wakuu kumi na mbili kati yao: As´ad bin Zaraarah bin ´Uds, Sa´d bin ar-Rabiy´ bin ´Amr, ´Abdullaah bin Rawaahah bin Tha´labah bin Imr’-il-Qays, Raafi´ bin Maalik bin al-´Ajlaan, al-Baraa’ bin Ma´ruur bin Sakhr bin Khansaa’, ´Abdullaah bin ´Amr bin Haraam (babake Jaabir) ambaye alisilimu usiku huo huo, Sa´d bin ´Ubaadah bin Dulaym, al-Mundhir bin ´Amr bin Khunays na ´Ubaadah bin as-Swaamit. Hawa tisa walikuwa ni kutoka al-Khazraj. Watatu kutoka al-Aws ilikuwa ni: Usayd bin al-Hudhayr bin Simaak, Sa´d bin Khaythamah bin al-Haarith na Rifaa´ah bin ´Abdil-Mundhir bin Zubayr. Imesemwa pia kuwa Abuul-Haytham bin at-Tayyihaan ndio alikuwa badala yake.

Wanawake wawili hao ilikuwa ni Umm ´Umaarah Nasiybah bint Ka´b bin ´Amr ambaye mvulana wake Habiyb bin Zayd bin ´Aasim bin Ka´b aliuawa na al-Musaylamah na Asmaa’ bint ´Amr bin ´Adiyy bin Naabiy.

Wakati bay´ah hii ilipotimia wakamuomba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) idhini kuwashambulia wale wengine ´Aqabah, lakini hakuwapa idhini hiyo. Badala yake akawapa idhini waislamu wa Makkah kuhamia al-Madiynah. Watu wakafanya hivo na mtu wa kwanza kuhama kwenda al-Madiynah alikuwa ni Abuu Salamah bin ´Abdil-Asad na mke wake Umm Salamah. Lakini njiani Umm Salamah akazuiwa na hivyo hakuweza kuwa pamoja naye kwa mwaka mmoja. Mvulana wake pia akachukuliwa. Baada ya mwaka mmoja akamchukua mvulana wake na wakasafiri kwenda al-Madiynah, ´Uthmaan bin Talhah akaandamana naye. Inasemekana pia kuwa Abuu Salamah alihama naye kabla ya bay´ah ya ´Aqabah ya pili na Allaah ndiye anajua zaidi. Kisha baada ya hapo watu wakahama mmoja baada ya mwingine.

[1] al-Bukhaariy (2808).

  • Mhusika: Imaam Ismaa´iyl bin Kathiyr ad-Dimashqiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Fusuwl fiy Siyrat-ir-Rasuwl, uk. 29-32
  • Imechapishwa: 18/03/2017