´Arshi kilugha ni kiti cha mfalme. Allaah (Ta´ala) amesema kuhusu Yuusuf:

وَرَفَعَ أَبَوَيْهِ عَلَى الْعَرْشِ

“Aliwainua wazazi wake wawili juu ya kiti cha ufalme.”[1]

Vilevile Amesema kuhusu malkia wa Saba´:

وَلَهَا عَرْشٌ عَظِيمٌ

“Na anacho kiti cha ufalme kikubwa.”[2]

Kuhusiana na ´Arshi ya Mwingi wa Rahmah ambayo amelingana juu yake, ni ´Arshi kubwa yenye kuwazunguka viumbe. ´Arshi ndio kiumbe kikubwa kabisa. Abu Dharr (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mbingu saba na ardhi saba ukizilinganisha na Kursiy ni kama mfano wa pete iliyotupwa kwenye jangwa. Na tofauti kati ya ´Arshi na Kursiy ni kama tofauti kati ya jangwa na pete hiyo.”[3]

Mtunzi wa kitabu Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema katika “ar-Risaalah al-´Arshiyyah”:

“Hadiyth hii ina njia nyingi. Imepokelewa na Abu Haatim, Ibn Hibbaan katika “as-Swahiyh”, Ahmad katika “al-Musnad” na wengineo.

Maana ya al-Kursiy kilugha ni kiti ambacho mtu hukaa juu yake. Ama Kursiy ambayo Allaah amejinasibishia nayo ni mahali pa kuwekea miguu Yake miwili (Ta´ala). Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Kursiy ni mahala pa kuwekea miguu miwili na ´Arshi hakuna awezaye kuikadiria isipokuwa Allaah (´Azza wa Jall).”[4]

Maana hii iliyotajwa na Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ndio yenye kutangaa kwa Ahl-us-Sunnah. Hii ndio sahihi kutoka kwake tofauti na mapokezi yaliyopokelewa yenye kusema kuwa Kursiy maana yake ni elimu. Kadhalika tafsiri ya al-Hasan al-Baswriy yenye kusema kuwa Kursiy maana yake ni ´Arshi ni dhaifu kwa mujibu wa Ibn Kathiyr (Rahimahu Allaah)[5].

[1] 12:100

[2] 27:23

[3] Ibn Hibbaan (94 – al-Mawaarid), Abu Nu´aym katika ”al-Hilyah” (1/167) na al-´Adhwamah (2/569, 649).

[4] al-Haakim amesema:

”Ni Swahiyh juu ya sharti za al-Bukhaariy na Muslim.” (al-Mustadrak (2/282))

adh-Dhahabiy amesema:

”Wapokezi wake ni waaminifu.” (al-´Uluww, uk. 61)

al-Azhariy amesema:

“Wanachuoni wameafikiana juu ya usahihi wa upokezi huu.” (Tahdhib-ul-Lughah (10/61))

[5] Tafsiyr-ul-Qur-aan al-´Adhwiym (1/311). Linganisha na Fath-ul-Baariy (8/199).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyah, uk. 45
  • Imechapishwa: 14/01/2020