Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Msingi wa tatu ni kumtambua Mtume wenu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). 

MAELEZO

Msingi wa tatu – Bi maana miongoni mwa misingi mitatu. Kwa sababu Shaykh (Rahimahu Allaah) mwanzoni wa kitabu ametaja kwamba ni wajibu kwa kila muislamu wa kike na wa kiume kujifunza misingi hii mitatu; kumjua Allaah, kuijua dini ya Uislamu na kumjua Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa dalili. Kuhusu msingi wa kwanza na msingi wa pili tayati tumekwishatangulia kutaja maelezo, ubainifu na dalili zake.

Msingi wa tatu ni kumjua Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wakati ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa mkatikati baina ya Allaah na viumbe Wake katika kufikisha dini na ujumbe wake basi ikawa ni lazima kumjua (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Vinginevyo ni vipi utamfuata mtu ilihali humjui? Ni lazima umjue kwa njia ya jina, nchi aliyozaliwa na kukulia, nchi aliyohamia na ujue muda wa umri wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Vigawanyo vya umri wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)  na vigawanyo vya muda ambao aliishi katika dunia hii. Unatakiwa vilevile umjue kabla ya kupewa utume na baada ya hapo, kabla ya kuhajiri na baada ya kuhajiri na pia ujue ni vipi alianza kwa Wahy (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ilikuwa wakati gani, ni Aayah zipi zinazofahamisha juu ya unabii wake, ni Aayah zipi zinazofahamisha juu ya utume wake na kutumilizwa kwake. Ni lazima uyajue mambo haya. Unapaswa kujua nasaba yake na anatokana na kabila gani. Kwa sababu waarabu wako makabila mengi. Hapana shaka kwamba yeye ni mwarabu. Ni lazima uyajue mambo haya juu ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa njia ya wewe kuzidurusu Aayah na Hadiyth zilizofungamana na mambo haya na uisome historia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ulinganizi wake. Lengo ni ili wewe uyajue mambo haya juu ya Mtume wako ambaye wewe umeamrishwa kumfuata na kumwigiliza.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 241-243
  • Imechapishwa: 03/02/2021