Kutokana na haya tunadhihirikiwa na ubatilifu wa uchawi na kwamba ni kufuru kubwa inayomtoa mtu nje ya dini, ni kuritadi kutoka katika Uislamu, kwamba ni katika mambo yanayovunja Uislamu na kwamba adhabu ya mwenye nao ni kuuawa kwa hali yoyote ile. Kuanzia hapa tunapata kutambua kuwa ile michezo ya sarakasi ya mazingaombwe inayofanywa katika sherehe na katika utalii ni uchawi wa wazi. Haijali kitu hata kama michezo hiyo itapewa majina mbalimbali kinyume na uhalisia wake.

Jengine ni kwamba tunapata kutambua kuwa haifai hakuwakubali wachawi katika jamii za Kiislamu kwa aina zote. Kwa sababu wakati mwingine wanakuja kwa aina ya kwamba wamekuja kutibu magonjwa na wanaita kuwa ni ´tiba ya wananchi` ilihali ni uchawi. Wakati mwingine wanakuja kwa aina ya kufanya Ruqyah ilihali uhakika wa mambo ni wachawi. Tatizo ni kwamba kuna wajinga ambao wanawaita ´Mashaykh na kwamba wametoka kusomewa kwa Mashaykh` ilihali ni wachawi. Lakini watu wa kawaida wanaamini kuwa ni Mashaykh na matabibu.

Vilevile haijuzu kutumia uchawi kwa jina la michezo ya sarakasi au michezo mfano wa hiyo, kama wale ambao wanaonyesha kuwa eti anaendesha gari kwenye nywele za mtu, eti gari linapita juu yake na halimdhuru, eti unachukuliwa msumari na anadungwa nao na haumdhuru, anajidunga kisu au eti anakula moto mbele za watu, matendo yote haya ni uchawi aina ya kiinimacho. Haifai kuutendea kazi, kuuridhia au kuwaleta wenye kufanya hivo wafanye mbele za waislamu. Ni maovu ya wazi kabisa. Kwa hivyo ni wajibu kuyakaripia, kuwachukulia hatua na kuitakasa miji ya waislamu kutokamana na hayo.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 151-152
  • Imechapishwa: 04/02/2019