118. Ishi katika dunia hii kama mgeni au mpita njia

Allaah (Ta´ala) amesema:

قُلْ مَتَاعُ الدُّنْيَا قَلِيلٌ وَالْآخِرَةُ خَيْرٌ لِّمَنِ اتَّقَىٰ وَلَا تُظْلَمُونَ فَتِيلًا

“Sema: “Starehe za dunia ni chache; na Aakhirah ni bora zaidi kwa mwenye kumcha Allaah na wala hamtodhulumiwa kadiri ya uzi wa kokwa ya tende.” 04:77

Kustarehe na dunia ni jambo dogo na kuburudika kwako kidogo kuliko kidogo. Thawabu za Aakhirah ndio kheri na bora kwa yule kuyaepuka maasi na kumtii Allaah.

Mtu anatakiwa kutambua kuwa mlango huu ni miongoni wa milango yenye manufaa zaidi kwa yule mwenye kuuzingatia. Dunia hii itaisha na kutoweka. Dunia hii ni sehemu ya mitihani. Ina tabu na mitihani, starehe za udanganyifu na majaribio. Usihuzunike kwa yale yaliyopitika kutoka kwayo. Usifurahie yale uliyopata kutoka kwayo. Usikate tamaa pindi mtoto au mtu anapokufa. Usihuzunike kwa kitu kilichokupita.

al-Bukhaariy amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) aliyesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alinishika kwenye mabega na kunambia: “Ishi duniani kama mgeni au mpita njia.”

Ibn ´Umar alikuwa akisema:

“Ukifikisha jioni usitarajii kuwa utafikisha asubuhi. Ukifikisha asubuhi usitarajii kuwa utafikisha jioni. Chukua kutoka katika siha yako uyape maradhi yako na uchukue kutoka katika maisha yako uyape mauti yako.”

Wanachuoni wengi wamesema pindi walipokuwa wakiifasiri Hadiyth hii:

“Usiitegemei dunia hii. Usiifanyi kuwa ndio makazi ya milele. Usiizungumzishe nafsi yako kuwa utaishi ndani yake muda mrefu. Usiitilie umuhimu mkubwa. Usidanganyike nayo. Ni ghururi na udanganyifu. Usifungamane nayo kama ambavyo msafiri hafungamani na mji wa wengine usiokuwa mji wake. Usijishughulishe na kitu ndani yake kama ambavyo msafiri anayeikumbuka familia yake hajishughulishi na kitu njiani. Na Allaah ndiye mwenye kutakwa msaada.”

Sahl bin Sa´d as-Saa´idiy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Kuna mwanaume alikuja kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kusema: “Ee Mtume wa Allaah! Nielekeze katika jambo ambali nikilifanya Allaah atanipenda na watu watanipenda.” Akasema: “Ipe nyongo dunia Allaah atakupenda. Kuwa ni mwenye kuvipa nyongo vile vilivyoko kwa watu watu watakupenda.”

Ameipokea Ibn Maajah kwa mlolongo wa wapokezi mzuri na alama ya usahihi wake uko wazi.

Amepokea vilevile ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Lau dunia hii ingelikuwa na thamani mbele ya Allaah sawa na ubawa wa mbu basi Allaah asingelimpa kafiri hata kinywaji cha maji.”

Ameipokea at-Tirmidhiy ambaye amesema kuwa ni Swahiyh.

at-Tirmidhiy amepokea kupitia kwa Ka´b bin ´Iyaadhw aliyesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kila Ummah una mtihani na mtihani wa Ummah wangu ni pesa.”

at-Tirmidhiy amesema kuwa ni nzuri na Swahiyh.

Tambua ya kwamba yule mwenye kuipenda dunia hii anaidhuru Aakhirah yake na yule anayeipenda Aakhirah anaidhuru dunia yake. Kwa hiyo kipe kipaumbele kile kitachobaki kuliko kile kitachotoweka.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 242-243
  • Imechapishwa: 30/12/2016