Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Amesema: “Kisha akaondoka na tukatulia muda mrefu. Halafu akasema (Swallla Allaahu ´alayhi wa salalm): “Ee ‘Umar! Je, unamjua ni nani yule aliyekuwa akiuliza?” Nikajibu: “Allaah na Mtume Wake ndio wanajua zaidi.” Akasema Mtume: “Ilikuwa ni Jibriyl ambaye amekuja kuwafundisha Dini yenu.”

MAELEZO

Amesema: “Kisha akaondoka… – Huyu ambaye ameingia na kuuliza maswali haya ni Jibriyl (´alayhis-Salaam). Amekuja kwa umbile la mwanamme, kama alivyosifiwa, kwa lengo awafunze waliokuweko pale dini yao kwa njia ya swali na jibu. Hadiyth hii imefahamisha juu ya mambo matukufu yafuatayo:

1-  Dini imegawanyika katika ngazi tatu; Uislamu, imani na ihsaan. Kila ngazi iko juu zaidi kuliko ilio kabla yake na kwamba kila ngazi ina nguzo. Kuna nguzo za Uislamu, nguzo za imani na nguzo ya ihsaan ambayo ni moja.

2- Kuna faida ya kufunza kwa njia ya kuuliza na kujibu. Hii ni njia ya kufunza ambayo imefaulu. Njia kama hii iko karibu zaidi na kuzindua na kupokea elimu. Kwa sababu mtu anauliza na anajiandaa kupokea jawabu. Kisha anapewa jibu ambalo alikuwa analitarajia. Njia kama hii inakuwa ni yenye kuthibiti.

3- Katika Hadiyth kuna dalili yenye kuonyesha kuwa mwenye kuulizwa juu ya elimu na akawa hajui basi anatakiwa kusema kuwa Allaah na Mtume Wake ndio wajuzi zaidi. Aitegemeze elimu kwa mwenye nayo. Asizungumzie jibu ilihali halijui au akakurupuka, mambo ambayo hayajuzu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati alipoulizwa kuhusu Qiyaamah akasema kuwa si yeye wala muulizaji wote wawili hawajui. Pia wakati alipowauliza Maswahabah kama wanamjua ni nani alikuwa muulizaji wakajibu kuwa Allaah na Mtume Wake ndio wanajua zaidi. Ni dalili yenye kufahamisha kuwa maswala ya Shari´ah na maswala ya dini haijuzu kuyakurupukia. Kwa sababu kufanya hivo ni kujikakama. Lakini ambaye ana elimu basi ajibu. Asiyekuwa na elimu aseme kuwa Allaah ndiye anajua zaidi.  Mwenye kusema kuwa hajui basi amejibu.

Imaam Maalik (Rahimahu Allaah) aliulizwa maswali arubaini ambapo akajibu masita katika hayo na akasema kuwa hajui kuhusu mengine. Muulizaji akamwambia: “Mimi nimetokea sehemu fulani, nimesafiri na nimemchokesha mnyama wangu na wewe unasema kuwa hujui!” Panda mnyama wako na wende katika mji wako ulikotokea na useme kuwa umemuuliza Maalik ambapo akajibu kuwa hajui. Hii sio aibu mtu akiwa hajui jawabu katika mambo ya dini kwamba akasema kuwa hajui ijapokuwa ni mwenye kujua. Isitoshe Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema:

“Muulizwaji si mjuzi kama asivyo vilevile muulizaji.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati mwingine alikuwa akiulizwa baadhi ya maswali na bado hajateremshiwa Wahy kutoka kwa Allaah (´Azza wa Jall) basi anasubiri mpaka Allaah amteremshie Wahy. Ni mara ngapi nasoma: “Wanakuuliza juu ya kadhaa na kadhaa” sema: “Kadhaa.”?

يَسْأَلُونَكَ عَنِ الْخَمْرِ وَالْمَيْسِرِ ۖ قُلْ فِيهِمَا إِثْمٌ كَبِيرٌ

”Wanakuuliza kuhusu pombe na kamari. Sema: “Katika viwili hivyo mna dhambi kubwa.”[1]

يَسْأَلُونَكَ عَنِ الْأَهِلَّةِ ۖ قُلْ هِيَ مَوَاقِيتُ لِلنَّاسِ وَالْحَجِّ

”Wanakuuliza juu ya miandamo ya mwezi. Sema: ”Hiyo ni vipimo vya nyakati kwa watu na hajj.”[2]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anapoulizwa na hana jibu basi anasubiri mpaka anapoteremshiwa Wahy kutoka kwa Allaah (´Azza wa Jall). Kadhalika wengine wana haki zaidi ya kusubiri mpaka kwanza wawaulize wengine au wengine wayatafiti masuala hayo katika vitabu vya wanachuoni mpaka wafikie jibu. Ama mtu kufanya papara ndani yake kuna khatari kubwa. Jengine ni utovu wa adabu kwa Allaah (´Azza wa Jall). Kwa sababu mwenye kujibu anajibu juu ya Shari´ah ya Allaah na anasema kuwa Allaah amehalalisha kadhaa na ameharamisha kadhaa au kwamba ameweka Shari´ah ya kadhaa. Kwa hiyo jambo hili ni lenye khatari mno.

4- Katika Hadiyth kuna dalili juu ya adabu za mwanafunzi. Jibriyl, ambaye ndiye bwana wa Malaika, anakaa mbele ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na huku ameweka magoti yake karibu na magoti ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akaweka viganja vyake juu ya mapaja yake. Kisha akauliza kwa adabu. Yote haya ni kwa ajili ya kuwafunza watu ni vipi wanatakiwa kufanya adabu pamoja na wanachuoni.

Haya ni baadhi ya faida zinazofahamishwa na Hadiyth. Faida nyingine ni:

5- Ubainifu wa baadhi ya alama za Qiyaamah. Ametaja alama mbili; kijakazi kumzaa bibi yake. Baadhi ya wanachuoni wamesema maana yake ni kwamba katika zama za mwisho utovu wa nidhamu utakithiri mpaka msichana awe kama kwamba yeye ndiye bosi wa mama yake kwa njia ya kwamba anamwamrisha, anamkataza na anamfanyia ukali.

[1] 02:219

[2] 02:189

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 238-241
  • Imechapishwa: 03/02/2021