117. Dalili juu ya kwamba adhabu ya mchawi ni kuuawa na tawbah yake haikubaliwi

Shaykh (Rahimahu Allaah) amesema:

“… au kuwa radhi nao.”

Ikiwa hakujifunza nao na wala hakuufunza, lakini hata hivyo akawa radhi nao kwa njia ya kwamba asiukemee. Huyu pia anakufuru. Kwa kuwa mwenye kuridhia kufuru, basi amekufuru. Muumini anatakiwa kukataza ukafiri na wala asiridhike nao.

Kwa hivyo uchawi ni kufuru. Ni mamoja kujifunza nao, kuufunza, kuutumia na kuwa radhi nao. Mambo yote haya ni kufuru. Ni katika dalili zinazoonyesha kwamba ni wajibu kukataza uchawi, kuwakataza wachawi na kuwaondosha katika jamii ili wasieneze shari na ufisadi ndani yake. Kwa ajili hii zimepokelewa Hadiyth zinazofahamisha kuuawa kwa wachawi. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Adhabu ya mchawi ni kumpinga upanga.”[1]

Maswahabah wakaitendea kazi Hadiyth hii ambapo wakawaua wachawi kadhaa.

´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) aliwaandikia barua wafanyakazi wake:

“Auawe kila mchawi mwanaume na mchawi mwanamke.”[2]

“Mama wa waumini, Hafswah bint ´Umar, alimuua kijakazi wake aliyemfanyia uchawi.”[3]

Swahabah ambaye ni Jundub bin Ka´b alimuona mchawi anafanya mchezo  mbele ya kiongozi mmoja wa Banuu Umayyah ambapo anawaonyesha watu kwamba eti anamuua mtu kisha anampa uhai tena, anakata kichwa chake kisha anakirudisha – inahusiana na uchawi aina ya kiinimacho kama nilivyowaambieni – uhakika wa mambo ni kwamba hafanyi chochote isipokuwa haya ni mazingaombwe na kuwazuga kwa watu. Swahabah huyu Jundub bin Ka´b akamsogelea na kumpinga upanga hadi akakata kichwa chake na akasema:

“Akiwa ni mkweli basi aihuishe nafsi yake.”[4]

Kwa ajili Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

“Kuuawa kwa mchawi ni jambo limesihi kwa watu watatu katika Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam); ´Umar, Hafswah na Jundub bin Ka´b.”

Lau mchawi atadhihirisha kutubu basi tawbah yake haikubaliwi. Bali atatakiwa kusimamishiwa adhabu. Tawbah yake haiaminiki. Ni zandiki ambaye anaweza kudhihirisha tawbah na ndani ya moyo wake kukawa bado kuna uchawi. Hivyo anauawa kwa hali yoyote. Ikiwa ni mkweli katika kutubia kwake basi ni baina yake yeye na Allaah. Allaah (Jalla wa ´Alaa) anakubali tawbah yake baina yake yeye na Allaah. Ama sisi tunamsimamishia adhabu ya Kishari´ah na tunamuua kwa hali yoyote.

[1] Ameipokea at-Tirmidhiy (1460), at-Twabaraaniy (1665), ad-Daaraqutwniy (04/114), al-Haakim (04/360) na wengineo.

[2] Ameipokea Ahmad (1657) na Abu Daawuud (3043). ´Allaamah Sulaymaan bin ´Abdillaah amesema:

“Cheni ya wapokezi wake ni nzuri.” (Taysiyr-ul-´Aziy al-Hamiyd (390)).

[3]Ameipokea ´Abdullaah bin Imaam Ahmad katika “al-Masaa-il” kutoka kwa baba yake (1543 na al-Bayhaqiy katika “al-Kubraa” (16967). Ni Swahiyh kwa mujibu wa Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab katika “Kitaab-ut-Tawhiyd”.

[4] Ameipokea al-Bukhaariy katika “at-Taariykh al-Kabiyr (2/222) na al-Bayhaqiy (1690). Ni Swahiyh kwa mujibu wa Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab katika “Kitaab-ut-Tawhiyd”.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 150-151
  • Imechapishwa: 31/01/2019