117. al-´Ayyaashiy upotoshaji wake wa kwanza wa al-An´aam

al-´Ayyaashiy amesema:

“Zaraarah na Humraan ameeleza kuwa Abu Ja´far na Abu ´Abdillaah amesema kuhusiana na maneno Yake:

وَأُوحِيَ إِلَيَّ هَـٰذَا الْقُرْآنُ لِأُنذِرَكُم بِهِ وَمَن بَلَغَ

“Nimeteremshiwa Wahy hii Qur-aan ili nikuonyeni kwayo na kila itakayomfikia.”[1]

“Bi maana maimamu baada yake. Na wao wanawaonya watu kwayo.”

Abu Khaalid al-Kaabuliy amesema: “Nilimuuliza Abu Ja´far kuhusiana na:

وَأُوحِيَ إِلَيَّ هَـٰذَا الْقُرْآنُ لِأُنذِرَكُم بِهِ وَمَن بَلَغَ

“Nimeteremshiwa Wahy hii Qur-aan ili nikuonyeni kwayo na kila itakayomfikia.”

ni kipi kinachomaanishwa juu ya hilo. Akasema: “Wale wasii ambao wanafikiwa kuwa imamu. Huyo anaonya kwa Qur-aan kama ambavyo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alivyoonya kwayo.”

´Abdullaah bin Bukayr amepokea kutoka kwa Muhammad, kutoka kwa Abu Ja´far aliyesema:

وَمَن بَلَغَ

“… na kila itakayomfikia.”

“Huyo ni ´Aliy.”[2]

 Suurah “al-An´aam” imeteremshwa Makkah. Kwa mujibu wa tafsiri hii Qur-aan ilikuwa tayari imeshaanza kufungua njia kwa ajili ya madhehebu ya Raafidhwah huko Makkah. Allaah awauwe waongo! Allaah amewatakasa watukufu wawili hawa Abu Ja´far na Abu ´Abdillaah kutokamana na uongo huu mbaya na wa kipumbavu.

Katika Aayah hii tukufu Allaah (Ta´ala) anaeleza ya kwamba ujumbe wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni wenye kuenea na kwamba ni jumla kwa watu na majini. Wale majini, watu, waarabu, wasiokuwa waarabu, wekundu, weusi na weupe, ambao watafikiwa na Qur-aan tukufu na wakaielewa basi wamekwishasimamiwa na haki na hivyo hawana udhuru wowote. Ujumbe wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) sio maalum kwa Quraysh wala waarabu. Maonyo ya Qur-aan yanawagusa wakazi wa Makkah, wapambizoni mwake na wengine wote wanaofikiwa nayo. ash-Shawkaaniy amesema wakati alipokuwa anafasiri hiyo Aayah:

“Bi maana Allaah amekuteremshieni Qur-aan hii, ambayo nakusomeeni nayo, ili niweze kuwatahadharisheni nayo na kuwatahadharisha wale wote itayowafikia huko mbeleni. Katika Aayah hii kuna dalili juu ya kwamba hukumu za Qur-aan ni zenye kutumika kwa wale wataokuwepo huko katika mustakabali, kama ambavyo zilifanya kazi kwa wale waliokuwepo pindi inapoteremka.”[3]

Ni jambo liko wazi kabisa kwa yule anayefahamu lugha ya kiarabu ya kwamba neno “na kila” limeegemezwa kwenye “ili nikuonyeni kwayo”, na si kwamba wenye kutahadharisha ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ´Aliy na kizazi chake. Tafsiri ya Baatwiniy huyu anaharibu vibaya maana nzima ya Aayah. Malengo yao ni kwamba wanataka kumfanya ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) na maimamu kutoka katika kizazi chake ni washirika wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa njia maalum, na si kwamna wanaingia katika jumla ya wale wenye kuonya. Wanacholenga ni kwamba wao tu ndio waonyaji na si wengineo. Huku ni kumsomea uongo Allaah na ni kukipotosha Kitabu Chake. Kuhusu kufikisha ujumbe wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) sio kazi maalum inayofanywa na ´Aliy na wale wanaodaiwa kuwa ni wasii. Kila mmoja awe mwarabu na asiyekuwa mwarabu anayefikiwa na ujumbe wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi analazimika kuufikisha. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Fikisheni kutoka kwangu ijapokuwa Aayah moja.”

Yule anayefikiwa na kitu kutoka katika ujumbe wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ingawa itakuwa ni Aayah moja, basi anawajibika kukifikisha. Allaah amewasifu Ummah huu kwa njia kubwa kabisa pale aliposema:

كُنتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ تَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَتَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَتُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ

“Mmekuwa Ummah bora kabisa ulioteuliwa kwa watu: mnaamrisha mema na mnakataza maovu na mnamuamini Allaah.”[4]

Huku ndio kufikisha kwao ujumbe wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Miongoni mwa kuamrisha mema ni kulingania katika Tawhiyd na kumtakasia Yeye nia na miongoni mwa kukataza maovu ni kukataza vilevile shirki, Bid´ah na upotevu.

Katika maneno yake haya kuna kuwatukana vilevile maimamu. Je, ni kweli kwamba walisimama na kazi ya kuwafikishia ujumbe majini na watu ulimwenguni kote? Maimamu ni sehemu katika Ummah ambao umefikisha ujumbe wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ulimwenguni kote na ukapambana katika njia ya Allaah. Wengi katika wao walikufa wakiwa mashahidi wakati walipokuwa wakifikisha ujumbe huu.

[1] 06:19

[2] Tafsiyr al-´Ayyaashiy (1/356).

[3] Fath-ul-Qadiyr (2/132).

[4] 03:110

  • Mhusika: Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Intiswaar li Kitaab-il-´Aziyz al-Jabbaar, uk. 174-175
  • Imechapishwa: 10/05/2018