Ni lazima kwa mtu ajue kuwa madhehebu ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah kuanzia waliotangulia na waliokuja nyuma ni kwamba kila mmoja anayekufa ilihali anamuabudu Allaah peke yake ni mwenye kudhaminiwa kuingiwa Peponi kwa hali yoyote ile.

Watu waliosalimika na maasi kama watoto, wendawazimu waliotokwa na akili baada tu ya kubaleghe, watu wenye kutubia tawbah ya kweli kutokamana na shirki na dhambi nyenginezo na baadaye wasitendi dhambi tena baada ya kutubia na ambaye amekulia katika kumuabudu Allaah pasi na kutenda dhambi, wote hawa wataingia Peponi na hawatotumbukia Motoni. Lakini hata hivyo watapita juu yake kutokamana na tofauti inayojulikana juu ya suala hili. Maoni sahihi – Allaah akitaka – juu ya kupita الورود ni kwamba kila mmoja atapita juu ya Njia ya Motoni, kama walivyosema wanachuoni wengi. Tunamuomba Allaah atukinge na joto na baridi yake.

Kuhusu watenda madhambi waliokufa baada ya kutenda madhambi makubwa ambayo hawakutubia kwayo, Allaah ana khiyari nini cha kuwafanya. Akitaka kuwaadhibu atawaadhibu kiasi cha madhambi yao kisha baadaye awaingize Peponi. Na akitaka atawasamehe kabisa. Kwa msemo mwingine ni kwamba hakuna yeyote aliyekuwa akimpwekesha Allaah atayedumishwa Motoni milele. Haijalishi kitu yale madhambi aliyofanya. Hii ni faraja bora kabisa kwa yule aliyefiliwa na nduguye au rafiki yake mtenda madhambi na hajui kuwa alitubia au hakutubia. Abu Zakariyyah an-Nawawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Kuna dalili kutoka katika Qur-aan, Sunnah na maafikiano yenye kuzingatiwa juu ya kanuni hii. Kumepokelewa maandiko mengi kabisa juu ya suala hili yanayopelekea jambo hili kuwa ni lenye kukata.”

Yanayotilia nguvu hili ni Hadiyth Swahiyh iliyopokelewa na ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kufa ilihali anajua kuwa hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah ataingia Peponi.”

al-Qaadhwiy ´Iyaadhw amesema:

“Watu wametofautiana juu ya waislamu watenda madhambi. Murji-ah wanasema kuwa hawadhuriki kwa maasi wakiwa ni waumini. Khawaarij wanasema kuwa yanamdhuru na kwamba amekufuru. Mu´tazilah wanasema kuwa atadumishwa Motoni milele ikiwa alifanya dhambi kubwa na kwamba haitakiwi kumwita muumini wala kafiri, bali [anatakiwa kuitwa] mtenda dhambi (Faasiq). Kundi la wanachuoni wanasema kuwa ni muumini hata kama hakusamehewa na hata kama ataadhibiwa kabla au baada na kuingia Peponi. Hadiyth hii ni hoja dhidi ya Khawaarij na Mu´tazilah. Ama kuhusu Murji-ah, hata kama wanatumia hoja kwa udhahiri wa Hadiyth tunasema kuwa inatakiwa kufasiriwa kuwa mtenda dhambi atasamehewa na kutoka Motoni kupitia uombezi na baadaye kuingia Peponi. Hivyo itakuwa maana ya maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayh iwa sallam): “ataingia Peponi” bi maana baada ya kuadhibiwa. Ni lazima Hadiyth ifasiriwe hivyo kwa kuwa kuna dalili nyingi zilizo wazi zinazofahamisha kuwa kuna baadhi ya watenda madhambi wataoadhibiwa.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 236-137
  • Imechapishwa: 27/12/2016