116. Aina tatu ya alama za Qiyaamah


Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Akasema: “Nieleze kuhusu alama zake!” Akasema: “Kijakazi kumzaa bibi yake

MAELEZO

Akasema: “Nieleze kuhusu alama zake!” – Bi maana alama zinazojulisha juu ya kukaribia kusimama kwake. Qiyaamah kina alama zake. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amezibainisha. Miongoni mwazo ni alama ndogondogo, alama kubwakubwa na alama za kati na kati. Zipo pia alama zenye kukaribia Qiyaamah ambazo zitakuwa wakati wa kusimama Qiyaamah. Alama nyenginezo ni zenye kutangulia.

Wanachuoni wamesema kuwa alama za Qiyaamah zimegawanyika aina tatu:

1- Alama ndogondogo zenye kutangulia.

2- Alama za kati na kati.

3- Alama kubwakubwa.

Alama ndogondogo na alama za kati na kati zote au baadhi yake zimekwishatangulia.

Kuhusu alama kubwakubwa kama kujitokeza kwa ad-Dajjal, kuteremka kwa ´Iysaa (´alayhis-Salaam), kujitokeza mnyama, kujitokeza kwa Ya´juuj na Ma´juuj. Hizi zitakuwa wakati wa kusimama kwa Qiyaamah.

Akasema: “Nieleze kuhusu alama zake!” – Wakati ambapo alama zilikuwa ni zenye kujulikana ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamjibu kwa kusema:

“Kijakazi kumzaa bibi yake.”

Hii ni moja katika alama za Qiyaamah. Kijakazi ni mwenye kumilikiwa na bibi yake ndiye bosi wake.

Wapambanuzi wamesema kuwa maana yake – na Allaah ndiye mjuzi zaidi – ni kwamba katika zama za mwisho kuwajamii wajakazi kutafanywa kwa wingi. Msichana huyo atakuwa huru na atakuwa ni bibi wa mama yake na mwenye kummiliki.

Kuna maoni mengine yenye kusema kuwa maana yake ni kwamba utovu wa nidhamu utakuwa mwingi na msichana atakuwa kama kwamba yeye ndiye bibi wa mama yake.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 236-237
  • Imechapishwa: 02/02/2021