115. Yote haya ni haki na mimi ni mwenye kuonelea hivo

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Ama masuala mengine kwamba nimesema:

“Uislamu wa mtu hautimii mpaka atambue maana ya “Laa ilaaha illa Allaah”, kwamba namtambua yule anayekuja na maana yake, kwamba namkufurisha mweka nadhiri pale anapokusudia kwa nadhiri yake kujikurubisha kwa asiyekuwa Allaah na akachukua nadhiri kwa sababu hiyo na kwamba kuchinja kwa mwengine asiyekuwa Allaah ni kufuru na kichinjwa hicho ni haramu.”

Masuala haya ni haki na mimi ni mwenye kuonelea hivo. Nina dalili juu yake kutoka katika maneno ya Allaah, maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na maneno ya wanachuoni wenye kufuatwa; kama maimamu wanne. Allaah akifanya wepesi basi nitapambanua jibu juu ya hayo katika kijitabu cha kujitegemea.

Kisha tambueni na zingatieni maneno Yake (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن جَاءَكُمْ فَاسِقٌ بِنَبَإٍ فَتَبَيَّنُوا أَن تُصِيبُوا قَوْمًا بِجَهَالَةٍ فَتُصْبِحُوا عَلَىٰ مَا فَعَلْتُمْ نَادِمِينَ

“Enyi walioamini! Anapokujieni fasiki kwa habari yoyote, basi pelelezeni msije mkawasibu watu kwa ujinga, mkawa kuwa wenye kujuta juu ya ambayo mmeyafanya.”[1]

MAELEZO

Uislamu wa mtu hautimii mpaka atambue… – Haya ni kweli. Shaykh (Rahimahu Allaah) anawafunza watu maana ya “Laa ilaaha illa Allaah” kwamba ni hakuna mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na wengineo ´ibaadah zao ni batili na shirki. Je, Shaykh analaumiwa kwa haya? Jibu ni hapana. Huu ndio mfumo wa Mitume.

Kwamba namkufurisha mweka nadhiri… – Haya pia ni kweli. Mwenye kuweka nadhiri kwa mwengine asiyekuwa Allaah ni kafiri. Kwa sababu amefanya aina moja wapo ya ´ibaadah kumfanyia mwengine asiyekuwa Allaah. Kwa hiyo hakuna lawama kwa Shaykh wala mwengine anapokufurisha kwa ajili hiyo.

Kwamba kuchinja kwa mwengine asiyekuwa ni kufuru – Ni kweli. Amesema (Ta´ala):

قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ لَا شَرِيكَ لَهُ

“Sema: “Hakika swalah yangu, kichinjwa changu, uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allaah pekee, Mola wa walimwengu, hali ya kuwa hana mshirika.”[2]

Katika Sunnah imekuja:

“Allaah amemlaani mwenye kuchinja kwa asiyekuwa Allaah.”[3]

Maneno yake:

“… na kichinjwa hicho ni haramu.”

Kwa sababu ni miongoni mwa vilivyofanywa halali kwa mwengine asiyekuwa Allaah. Allaah (Jalla wa ´Alaa) anasema:

وَلَا تَأْكُلُوا مِمَّا لَمْ يُذْكَرِ اسْمُ اللَّـهِ عَلَيْهِ

“Wala msile katika ambavyo havikutajiwa jina la Allaah.”[4]

حُرِّمَتْ عَلَيْكُمُ الْمَيْتَةُ وَالدَّمُ وَلَحْمُ الْخِنزِيرِ وَمَا أُهِلَّ لِغَيْرِ اللَّـهِ بِهِ

“Mmeharamishiwa nyamafu na damu na nyama ya nguruwe na kilichotajiwa lisilokuwa jina la Allaah katika kuchinjwa kwake.”[5]

Maneno yake:

“Masuala haya ni haki na mimi ni mwenye kuonelea hivo.”

Kwa sababu ndivo inavopelekea Qur-aan na Sunnah. Kwa hivo hakuna lawama zozote kwa Shaykh. Bali anatakiwa kushukuriwa juu ya haya na kuombewa du´aa. Lakini wanazingatia mazuri kuwa ni mabaya.

Hapa ndipo mwisho wa kitabu hichi kilichobarikiwa. Allaah ndiye anajua zaidi. Swalah na salamu zimwendee Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake. Himdi zote anastahiki Allaah, Mola wa walimwengu.

Imekamilika katika 18/01/1426

[1] 49:06

[2] 06:162-163

[3] Muslim (1978) kupitia kwa ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh).

[4] 06:121

[5] 05:03

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 159-160
  • Imechapishwa: 10/06/2021