115. Mwabudu Allaah kama vile anakuona vinginevyo tambua kuwa Yeye anakuona

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Akasema: “Nielezee kuhusu Ihsaan!” Akasema: “Ni kumuabudu Allaah kama vile unamuona. Ikiwa wewe humuoni, basi Yeye Anakuona.” Akasema: “Nieleze kuhusu Qiyaamah.” Akasema: “Muulizwaji si mjuzi kama asivyo vilevile muulizaji.” 

MAELEZO

Akasema: “Nielezee kuhusu Ihsaan!” – Imekwishatangulia kwamba mtenda ihsaan ni yule anayemwabudu Allaah kwa kumuona Allaah na yakini kama vile anamuona Allaah au amwabudu Allaah kwa kujua kuwa Allaah anamuona na hivyo akifanye vizuri kitendo chake kwa sababu Allaah anamuona. Mtenda ihsaan anamwabudu Allaah ima kwa kumuona Allaah ndani ya moyo, hali ambayo ndio kamilifu zaidi, au kwa kujua kuwa Allaah anamchunga na atambue kuwa Allaah anamuona kila mahali au katika kitendo chochote anachofanya. Hii ndio ihsaan.

Akasema: “Nieleze kuhusu Qiyaamah… – Nieleze Qiyaamah ni lini? Jibu hili hakuna yeyote anayejua jibu lake isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Kwa sababu kusimama kwa Qiyaamah hakuna yeyote anayejua kitakuwa lini isipokuwa Allaah (´Azza wa Jall).

Sisi tunajua kuwa Qiyaamah kitasimama. Hatuna mashaka juu ya jambo hilo. Mwenye kutilia shaka juu ya hili ni kafiri. Tunajua kuwa ni lazima Qiyaamah kisimame. Lakini hata hivyo Allaah (´Azza wa Jall) hakutwambia ni lini kitatokea Qiyaamah na wala hakutwambia. Ni jambo amelificha katika elimu Yake. Amesema (Ta´ala):

إِنَّ اللَّـهَ عِندَهُ عِلْمُ السَّاعَةِ

“Hakika Allaah Kwake ndiko kuna elimu ya Saa.”[1]

يَسْأَلُونَكَ عَنِ السَّاعَةِ أَيَّانَ مُرْسَاهَا ۖ قُلْ إِنَّمَا عِلْمُهَا عِندَ رَبِّي ۖ لَا يُجَلِّيهَا لِوَقْتِهَا إِلَّا هُوَ

”Wanakuuliza kuhusu Saa, ni lini kitatokea? Sema: ”Hakika ujuzi wake uko kwa Mola wangu. Hakuna wa kuidhihirisha wakati wake isipokuwa Yeye.”[2]

Yeye ndiye anakijua. Amesema (Ta´ala):

وَعِندَهُ مَفَاتِحُ الْغَيْبِ لَا يَعْلَمُهَا إِلَّا هُوَ

“Kwake zipo funguo za mambo yaliyofichikana; hakuna azijuaye isipokuwa Yeye tu.”[3]

Katika hayo ni wakati wa kusimama Qiyaamah.

Akasema: “Muulizwaji si mjuzi… – Mimi na wewe sote tunalingana hatujui ni lini kitasimama Qiyaamah. Allaah (Jalla wa ´Alaa) hakumfunulia yeyote jambo hili; si Malaika, Mitume wala mwengine yeyote. Bali ni jambo amelificha katika elimu Yake (Subhaanahu wa Ta´ala).

[1] 31:34

[2] 07:187

[3] 06:59

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 234-236
  • Imechapishwa: 02/02/2021