115. al-´Ayyaashiy upotoshaji wake wa tatu wa al-Maa-idah

al-´Ayyaashiy amesema wakati alipokuwa akifasiri maneno ya Allaah (Ta´ala) juu ya sehemu ya mawindo:

يَحْكُمُ بِهِ ذَوَا عَدْلٍ مِّنكُمْ

“…wahukumu wawili ambao ni waadilifu katika nyinyi.”

 “Zaraarah amesema: “Nilimuuliza Abu Ja´far juu ya maneno ya Allaah:

يَحْكُمُ بِهِ ذَاعَدْلٍ مِّنكُمْ

“…ahukumu ambaye ni mwadilifu katika nyinyi.”

ambapo akasema ambaye ni mwadilifu ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na maimamu baada yake.”

Halafu akasema:

“Hili ni kosa la mwandishi.”

Muhamad bin Muslim amepokea kutoka kwa Abu Ja´far aliyesema: “Bi maana mwanamume mmoja na ni imamu.”

Zaraarah amesema: “Nimemsikia Abu Ja´far akisema:

يَحْكُمُ بِهِ ذَاعَدْلٍ مِّنكُمْ

“…ahukumu ambaye ni mwadilifu katika nyinyi.”

“Huyo ni Mtume wa Allaah na maimamu baada yake. Hata hivyo imamu peke yake anatosheleza.”[1]

Mhakiki amerejesha kwa “al-Bihaar” na “al-Burhaan”.

Ndani ya maneno yake kuna yafuatayo:

1- Kukipotosha Kitabu cha Allaah pale anapodanganya na kusema “ambaye ni mwadilifu” badala ya “wawili ambao ni waadilifu”. Anakadhibisha maneno ya Allaah:

إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا الذِّكْرَ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ

“Hakika Sisi Tumeteremsha Ukumbusho na hakika Sisi bila shaka ndio Tutakaoihifadhi.”[2]

2- Hajali mgongano ulioko katika mapokezi mbalimbali. Mara aseme ambaye ni mwadilifu ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na maimamu na mara aseme ambaye ni mwadilifu ni mwanamume mmoja naye ni imamu.

3- Anabatilisha uadilifu wa Maswahabah na uadilifu wa waumini wengine wote mpaka siku ya Qiyaamah. Anafanya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na imamu pekee ndio wawezao kuhukumu juu ya sehemu ya mawindo. Hakuna dalili yoyote zaidi ya matamanio ya Baatwiniyyah. Baada ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Maswahabah walihukumu, na khaswa khaswa Abu Bakr na ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhum), kutokana na Aayah hii na kuenea kwake. Vilevile wanachuoni wa Ummah wamethibitisha hukumu hii inayoweza kutumika kwa kila mwadilifu mpaka siku ya Qiyaamah.

[1] Tafsiyr al-´Ayyaashiy (1/344).

[2] 15:09

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Intiswaar li Kitaab-il-´Aziyz al-Jabbaar, uk. 171-172
  • Imechapishwa: 24/04/2018