114. Ni lazima kwa mtu akusanye Uislamu na imani vyote viwili

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Kisha akasema: “Nieleze kuhusu imani!” Akasema: “Ni kumuamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Yake na siku ya Mwisho na kuamini Qadar; kheri na shari yake.” Akasema: “Umesema kweli!” 

MAELEZO

Akasema: “Nieleze kuhusu imani!”… – Akamkhabarisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) nguzo sita za imani baada ya kumtajia nguzo tano za Uislamu. Uislamu na imani vinapotajwa kwa pamoja basi Uislamu maana yake ni yale matendo yenye kuonekana na imani inakuwa ni yale matendo yaliyojificha ambayo yako moyoni na yanayosimama kwayo katika kusadikisha na elimu. Ni lazima kukusanya Uislamu na imani vyote viwili. Uislamu ni yale matendo ya uinje na imani ni yale matendo ya ndani. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Uislamu unakuwa waziwazi na imani inakuwa moyoni.”[1]

Vikitajwa vyote viwili kwa pamoja basi kila kimoja katika hivyo kinakuwa na maana yake. Kikitajwa kimoja basi kimoja kinaingia ndani ya kingine. Imani ikitajwa peke yake basi Uislamu unaingia ndani yake na Uislamu ukitajwa peke yake imani inaingia ndani yake. Kwa sababu Uislamu hausihi bila ya imani na wala imani haisihi bila ya Uislamu. Ni lazima yawepo yote mawili. Ni mambo mawili yenye kwenda sambamba. Kwa ajili hii wamesema kuwa Uislamu na imani ni katika majina ambayo yakikusanyika yanafarikiana na yakifarikiana yanakusanyika. Wanachomaanisha ni kwamba yanaingiliana kwa sababu ni yenye kwenda sambamba. Kimoja hakiachi kingine. Akamuuliza juu ya matendo ya nje na matendo ya ndani na akambainishia (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) nguzo za kila kimoja katika Uislamu na imani.

[1] Ahmad (19/374) (12381).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 233-234
  • Imechapishwa: 01/02/2021