114. Ikiwa Mtume alituhumiwa atasalimika kweli Ibn ´Abdil-Wahhaab?

Ikiwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhu wa sallam) alituhumiwa kwamba anamkufurisha al-Masiyh na eti anasema kuwa yuko Motoni kwa sababu manaswara wamemwabudu, vipi wasimtuhumu Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab?

Maneno yake:

“Wakamtuhumu tena eti yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anasema kuwa Malaika, ´Iysaa na ´Uzayr wako Motoni.”

Kwa sababu wameabudiwa badala ya Allaah. Kwani Aayah inasema:

إِنَّكُمْ وَمَا تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ حَصَبُ جَهَنَّمَ أَنتُمْ لَهَا وَارِدُونَ

”Hakika nyinyi na yale mnayoyaabudu badala ya Allaah ni mawakio ya moto wa Jahannam, nyinyi mtauingia.”[1]

Wakasema kuwa Aayah hii ni yenye kuenea na wanaingia pia Malaika, ´Iysaa, ´Uzayr na waja wengine wema. Jibu ni kwamba watu hawa hawakutaka waabudiwe badala ya Allaah. Bali walikuwa wakikaripia matendo hayo kipindi cha uhai wao. Kwa hiyo wataepushwa mbali na Moto:

لَا يَسْمَعُونَ حَسِيسَهَا ۖ وَهُمْ فِي مَا اشْتَهَتْ أَنفُسُهُمْ خَالِدُونَ

“Hawatosikia mvumo wake nao watadumu katika ambayo zimetamani  nafsi zao.”[2]

Ni ´Iysaa, ´Uzayr na wale waliotanguliwa na wema kutoka kwa Allaah. Hakika wao watatengwa mbali na Moto. Wakiabudiwa baada ya kufa kwao ni jambo haliwadhuru. Kwa sababu walikuwa wakiyakemea kipindi walipokuwa hai.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhu wa sallam) ameabudiwa baada ya kufa kwake. Makhurafi na washirikina wanamwabudu. Je, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhu wa sallam) anasemwa vibaya kwa matendo hayo au kusema kwamba Muhammad yuko Motoni kwa sababu ameabudiwa badala ya Allaah? Sivyo hivo. Kwa sababu alikuwa akiyakemea hayo katika uhai wake na akipambana kwa sababu hiyo. Ama kitendo cha yeye kuabudiwa baada ya kufa kwake lawama hazirudi kwake.

[1] 21:98

[2] 21:101-102

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 156-158
  • Imechapishwa: 16/06/2021