113. Jibu la Ibn ´Abdil-Wahhaab dhidi uongo wa Ibn Suwhaym na makhurafi wengine

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Jawabu langu juu ya masuala haya nikusema:

سبحانك هذا بهتان عظيم

“Kutakasika ni Kwako, hakika huu ni uzushi mkubwa!”

Kabla yake alituhumiwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) eti anamtukana ´Iysaa bin Maryam (´alayhimaas-Salaam) na eti anawatukana waja wema. Nyoyo zao zimefanana juu ya kuzua uongo na uzushi. Amesema (Ta´ala):

إِنَّمَا يَفْتَرِي الْكَذِبَ الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِآيَاتِ اللَّـهِ ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْكَاذِبُونَ

“Hakika si venginevyo wanaotunga uongo ni wale ambao hawaamini Aayah za Allaah na hao ndio waongo.”[1]

Wakamtuhumu tena eti yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anasema kuwa Malaika, ´Iysaa na ´Uzayr wako Motoni. Ndipo Allaah akateremsha kuhusu hilo:

إِنَّ الَّذِينَ سَبَقَتْ لَهُم مِّنَّا الْحُسْنَىٰ أُولَـٰئِكَ عَنْهَا مُبْعَدُونَ

“Hakika wale ambao umewatangulia wema Wetu hao watawekwa mbali nao [Moto].”[2]

MAELEZO

Mambo haya waliyozua amesema (Rahimahu Allaah) wakati wa kuyajibu:

سبحانك هذا بهتان عظيم

“Kutakasika ni Kwako, hakika huu ni uzushi mkubwa!”

Yote haya yaliyosemwa juu ya maneno haya ni uzushi mkubwa ambao haukusemwa na Shaykh. Ametakasika nao mbali – Allaah amrehemu rehema pana.

Maneno yake:

“Kabla yake alituhumiwa… “

Bi maana kabla ya Ibn Suwhaym. Makafiri na washirikina walimtuhumu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa hiyo yeye Ibn ´Abdil-Wahhaab ana kiigizo chema kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pindi anapotuhumiwa na Ibn Suwhaym. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alituhumiwa mambo makubwa kuliko haya.

Wamesema kuhusu Mtume kwamba anamtukana ´Iysaa bin Maryam. Hapo ilikuwa pale kulipoteremka maneno Yake (Ta´ala):

إِنَّكُمْ وَمَا تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ حَصَبُ جَهَنَّمَ أَنتُمْ لَهَا وَارِدُونَ

”Hakika nyinyi na yale mnayoyaabudu badala ya Allaah ni mawakio ya moto wa Jahannam, nyinyi mtauingia.”[3]

Wakasema kuwa Muhammad anamtukana ´Iysaa na mama yake. Kwa sababu ´Iysaa anaabudiwa badala ya Allaah na hiyo ina maana kwamba atatupwa Motoni:

وَقَالُوا أَآلِهَتُنَا خَيْرٌ أَمْ هُوَ

“Wakasema: “Je, waabudiwa wetu ni bora au yeye?”[4]

Wanamkusudia ´Iysaa (´alayhis-Salaam). Allaah akateremsha:

الَّذِينَ سَبَقَتْ لَهُم مِّنَّا الْحُسْنَىٰ أُولَـٰئِكَ عَنْهَا مُبْعَدُونَ لَا يَسْمَعُونَ حَسِيسَهَا ۖ وَهُمْ فِي مَا اشْتَهَتْ أَنفُسُهُمْ خَالِدُونَ

“Hakika wale ambao umewatangulia wema Wetu, basi hao watatenganishwa nao; hawatosikia mvumo wake nao watadumu katika ambayo zimetamani  nafsi zao.”[5]

Aayah inamlenga yule mwenye kuabudiwa hali ya kuwa yuko radhi. ´Iysaa hakuridhia na wala hakuwaamrishi wamwabudu. Bali aliwaamrisha wamwabudu Allaah (´Azza wa Jall):

مَا قُلْتُ لَهُمْ إِلَّا مَا أَمَرْتَنِي بِهِ أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ رَبِّي وَرَبَّكُمْ

”Sijawaambia isipokuwa yale uliyoniamrisha kwayo kwamba: ”Mwabuduni Allaah, Mola wangu na Mola wenu.”[6]

وَإِنَّ اللَّـهَ رَبِّي وَرَبُّكُمْ فَاعْبُدُوهُ ۚ هَـٰذَا صِرَاطٌ مُّسْتَقِيمٌ

”Na kwamba hakika Allaah ni Mola wangu na Mola wenu, hivyo basi mwabuduni Yeye pekee – hii ndio njia iliyonyooka.”[7]

´Iysaa (´alayhis-Salaam) hakuwaita watu wamwabudu yeye. Bali alikaripia kitendo hicho. Wale ambao wanawaita watu wawaabudu ndio ambao watakuwa Motoni pamoja na wale waliokuwa wakiwaabudu. Ama ´Iysaa, ´Uzayr na wengineo katika Mitume walikuwa wakikemea kitendo hichi katika uhai wao. Walipofariki ndipo watu wakafanya haya juu yao baada ya wao kufa. ´Iysaa (Swalla Allaahu ´alayhu wa sallam) alisema:

وَكُنتُ عَلَيْهِمْ شَهِيدًا مَّا دُمْتُ فِيهِمْ ۖ فَلَمَّا تَوَفَّيْتَنِي كُنتَ أَنتَ الرَّقِيبَ عَلَيْهِمْ ۚ وَأَنتَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ

”Lakini uliponipaisha juu ulikuwa Wewe ndiye Mwenye kuchunga juu yao; na Wewe juu ya kila jambo ni Mwenye kushuhudia.”[8]

Manabii, Mitume na waja wema hawaamrishi watu wawaabudu:

وَمَن يَقُلْ مِنْهُمْ إِنِّي إِلَـٰهٌ مِّن دُونِهِ فَذَٰلِكَ نَجْزِيهِ جَهَنَّمَ ۚ كَذَٰلِكَ نَجْزِي الظَّالِمِينَ

“Na yeyote yule miongoni mwao atasema: “Mimi ni mwabudiwa badala Yake, basi huyo Tutamlipa Jahannam. Hivyo ndivyo tunavyowalipa madhalimu.”[9]

مَا كَانَ لِبَشَرٍ أَن يُؤْتِيَهُ اللَّـهُ الْكِتَابَ وَالْحُكْمَ وَالنُّبُوَّةَ ثُمَّ يَقُولَ لِلنَّاسِ كُونُوا عِبَادًا لِّي مِن دُونِ اللَّـهِ

“Haiwi kwa mtu kwamba Allaah amempa Kitabu na hukuma na unabii kisha awaambie watu: “Kuweni wenye kuniabudu mimi badala ya Allaah.”[10]

Allaah akawatakasa Mitume kutokamana na maneno haya. ´Iysaa hakuwaambia wamwabudu. Walimwabudu baada ya kufa kwake. Kwa hiyo halaumiwi  (Swalla Allaahu ´alayhu wa sallam). Allaah akawaraddi kwa kusema:

الَّذِينَ سَبَقَتْ لَهُم مِّنَّا الْحُسْنَىٰ

“Hakika wale ambao umewatangulia wema Wetu… “

Anaingia pia ´Iysaa (Swalla Allaahu ´alayhu wa sallam):

أُولَـٰئِكَ عَنْهَا مُبْعَدُونَ لَا يَسْمَعُونَ حَسِيسَهَا ۖ وَهُمْ فِي مَا اشْتَهَتْ أَنفُسُهُمْ خَالِدُونَ

“… basi hao watatenganishwa nao; hawatosikia mvumo wake nao watadumu katika ambayo zimetamani  nafsi zao.”

Katika “az-Zukhruf” akasema:

وَلَمَّا ضُرِبَ ابْنُ مَرْيَمَ مَثَلًا إِذَا قَوْمُكَ مِنْهُ يَصِدُّونَ

“Na alipopigiwa mfano mwana wa Maryam, tahamaki watu wako wanaupigia kelele kuucheka.”[11]

Wakasema kwamba ikiwa waungu wako Motoni basi ´Iysaa pia atakuwa pamoja nao. Kwa sababu ni mwenye kuabudiwa badala ya Allaah. Wanachotaka ni kumjibu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhu wa sallam). Ndipo Allaah (Jalla wa ´Alaa) akasema:

مَا ضَرَبُوهُ لَكَ إِلَّا جَدَلًا ۚ بَلْ هُمْ قَوْمٌ خَصِمُونَ إِنْ هُوَ إِلَّا عَبْدٌ

“Hawakukupigia mfano huo isipokuwa tu kutaka ubishi. Bali wao ni watu makhasimu. Yeye si chochote isipokuwa ni mja.”[12]

Bi maana ´Iysaa (´alayhis-Salaam):

أَنْعَمْنَا عَلَيْهِ وَجَعَلْنَاهُ مَثَلًا لِّبَنِي إِسْرَائِيلَ

“… Tuliyemneemesha na tukamfanya ni mfano kwa wana wa Israaiyl.”[13]

Allaah akawaraddi sehemu mbili: katika Suurah “al-Anbiyaa´” na katika “Suurah az-Zukhruf”. Namna hii ndivo Qur-aan inawaraddi watu wa batili na inasambaratisha hoja zao baba.

[1] 16:105

[2] 21:101

[3] 21:98

[4] 43:58

[5] 21:101-102

[6] 05:117

[7] 19:36

[8] 05:117

[9] 21:29

[10] 03:79

[11] 43:57

[12] 43:58-59

[13] 43:59

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 155-156
  • Imechapishwa: 15/06/2021