Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Hakuwa na alama ya kuonesha kuwa ni msafiri na wala hapakuwa na hata mmoja katika sisi aliyemtambua. Alienda akakaa karibu na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaweka magoti yake karibu na magoti yake na akaweka viganja vyake juu ya mapaja yake.” Akasema: “Ee Muhammad, nieleze kuhusu Uislamu!”

MAELEZO

Hakuwa na alama… – Hapakuwa na hata mmoja katika wale waliokuweko pale ambaye alimtambua. Haya ni maajabu kwamba anaonekana kuwa amefika kutoka safarini mpaka watu waseme kuwa si katika wakazi wa pale Madiynah na pia hawamjui. Jengine ni kwamba hakuwa ni miongoni mwa wakazi wa pale mjini mpaka wamjue. Hali yake ikawachanganya kwamba haonekani amefika kutoka safarini na wala sio katika wakazi wa pale mjini. Angelikuwa ameonekana ametoka safarini basi kungelionekana kwake alama za safari katika nguo na rangi zake. Kwa sababu msafiri kunaonekana kwake alama za safari. Hakuna yeyote katika wale waliokuweko pale ambaye alikuwa anamjua; si katika wakazi wa pale mjini wala haonekani kuwa amefika kutoka safarini. Wakawa wanajiuliza: ametokea wapi bwana huyu ambaye anashangaza! Akakaa karibu na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mbele yake mkao wa mwanafunzi mbele ya mwalimu wake.

Akaweka magoti yake karibu na magoti ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ina maana kwamba alimsogelea sana.

Akaweka viganja vyake juu ya mapaja yake – Bi maana juu ya mapaja ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Akasema: “Ee Muhammad! – Alimzungumzisha kwa jina lake na wala hakusema “Ee Mtume wa Allaah!”. Pengine alifanya hivo (´alayhis-Salaam) ili Maswahabah wafikirie kuwa ni mtu wa kutoka shambani. Kwa sababu miongoni mwa ada za watu wa shambani walikuwa wakimzungumzisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa jina lake. Watu wa mashambani huwa juu ya tabia na yale waliyozowea. Isitoshe hiyo ni ziada ya mshangao na kupofusha ili wasiweze kumjua.

Akasema: “Ee Muhammad! – Nipe maelezo juu ya maana ya Uislamu.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 231-232
  • Imechapishwa: 01/02/2021