Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili kutoka katika Sunnah ni Hadiyth ya Jibriyl inayojulikana iliyopokelewa na ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesema:

“Siku moja tulipokuwa tumekaa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitutokea mtu ambaye nguo zake zilikuwa nyeupe pepe na nywele zake zilikuwa nyeusi sana.”

MAELEZO

Tumekwishatangulia kuzungumzia kuhusu Uislamu, imani na ihsaan na nguzo ya kila ngazi. Shaykh (Rahimahu Allaah) ametaja dalili za kila ngazi kutoka katika Qur-aan. Yote haya yamekwishatangulia na yamekwisha. Halafu Shaykh (Rahimahu Allaah) akataja dalili ya ngazi hizi kutoka katika Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akataja Hadiyth ya Jibriyl na kwamba alimjia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pindi alipokuwa na Maswahabah zake. Alimjia kwa umbile la mwanamme na akakaa karibu na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akamuuliza juu ya Uislamu, imani na ihsaan. Baada ya hapo akamuuliza kuhusu Qiyaamah na alama zake. Hii ndio inaitwa ´Haidyth ya Jibriyl au Hadiyth ya ´Umar´. Ni Hadiyth iliopokelewa kwa njia nyingi kutoka kwa idadi ya Maswahabah kadhaa. Ni Hadiyth ambayo ni Swahiyh. Shaykh (Rahimahu Allaah) akataja upokezi wa ´Umar bin al-Khattwaab[1] juu ya Hadiyth hii pamoja na utofauti katika matamshi ya Hadiyth kwenye njia zengine. Lakini hata hivyo maana yake ni moja.

Siku moja tulipokuwa tumekaa… – Ilikuwa ni katika mazowea yao (Radhiya Allaahu ´anhum) wakikusanyika kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) msikitini, wakipokea elimu kutoka kwake, wakisikiliza majibu yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya yale maswali wanayomuuliza. Walipokuwa katika hali hiyo kama kawaida, aliwazukia mtu ambaye nguo zake zilikuwa nyeupe pepe na nywele zake zilikuwa nyeusi sana. Alikuwa ni Jibriyl (´alayahis-Salaam) ambaye kajifananisha umbo la bwana huyu na hakuwajia katika umbo lake la Malaika kwa sababu hawawezi kustahamili kumuona akiwa na umbile lake la Malaika.

[1] Muslim (08) na al-Haakim (01/93).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 226-227
  • Imechapishwa: 28/01/2021