11. Wafuasi wa maimamu walikuwa tayari kuacha maoni yao kwa sababu ya Sunnah

Wafuasi wa maimamu walikuwa wanaendana japo:

ثُلَّةٌ مِّنَ الْأَوَّلِينَ وَقَلِيلٌ مِّنَ الْآخِرِينَ

“Kundi kubwa katika wa mwanzoni na wachache katika wa mwishoni.”[1]

Walikuwa hawachukui maoni ya maimamu wote. Bali mara nyingi wameyaacha maoni mengi pindi ilipodhihiri kuwa yanapingana na Sunnah. Maimamu wawili Muhammad bin al-Hasan na Abu Yuusuf (Rahimahumu Allaam) wametofautiana na mwalimu wao Abu Haniyfah takriban theluthi[2] ya maoni yake. Vitabu vya mataga ni vyenye kutolea ushahidi juu ya hilo. Mfano wa hayo yanasemekana vilevile kwa Imaam al-Muzaniy[3] na wafuasi wengineo wa ash-Shaafi´iy. Ni jambo lingechukua muda mrefu endapo tungetaja mifano yote. Kwa ajili hiyo tunatosheka na mifano ya watu wawili:

1- Imaam Muhammad[4] amesema:

“Abu Haniyfah (Rahimahu Allaah) alikuwa haonelei kuiambatanisha du´aa ya kuomba mvua pamoja na swalah. Kuhusu mimi, naona kuwa imamu anatakiwa kuwaswalisha watu Rak´ah mbili, aombe du´aa halafu aigeuze Ridaa´ yake.”[5]

2- ´Iswaam bin al-Balkhiy ambaye alikuwa ni mmoja katika maswahiba wa Imaam Muhammad na alikuwa ni katika wanafunzi wa karibu wa Imaam Abu Yuusuf[6]. Kwa vile hajui dalili yake, matokeo yake ilikuwa inatokea mara nyingi akifutu tofauti na maoni ya Abu Haniyfah kwa sababu amedhihirikiwa na dalili[7]. Hivyo akinyanyua mikono yake wakati wa kwenda katika Rukuu´ na wakati wa kuinuka kutoka katika Rukuu´[8].

Kwa kumalizia natarajia kuwa hatopatikana yeyote katika wale wenye kufuata kichwa mchunga ambaye atatukana mfumo wa kitabu hiki na kuacha kufaidika na Sunnah za kinabii kwa sababu tu hakiafikiani na madhehebu yao. Badala yake natarajia kuwa watazingatia nukuu za maimamu kuhusu uwajibu wa kuitendea kazi Sunnah na kuyaacha maoni yao yanayopingana nayo. Wanatakiwa kutambua kwamba kuponda mfumo wa kitabu hiki si jengine isipokuwa ni kuwaponda wale maimamu wao husika. Kwani tumechukua mfumo huu kutoka kwao. Yule mwenye kupuuzilia mbali suala hili basi yuko katika khatari kubwa. Kwa sababu hiyo ina maana kwamba anaipa mgongo Sunnah. Tumeamrishwa wakati wa kutofautiana kurejea na kutegemea Sunanh. Amesema (Ta´ala):

فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لَا يَجِدُوا فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُوا تَسْلِيمًا

“Basi naapa kwa Mola wako hawatoamini mpaka wakufanye wewe kuwa ni mwamuzi katika yale wanayozozana baina yao, kisha wasipate katika nyoyo zao uzito katika yale uliyohukumu na wajisalimishe kikamilifu kabisa.”[9]

Ninamuomba Allaah atujaalie miongoni mwa wale aliosema juu yake:

إِنَّمَا كَانَ قَوْلَ الْمُؤْمِنِينَ إِذَا دُعُوا إِلَى اللَّـهِ وَرَسُولِهِ لِيَحْكُمَ بَيْنَهُمْ أَن يَقُولُوا سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا ۚ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَيَخْشَ اللَّـهَ وَيَتَّقْهِ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَائِزُونَ

“Hakika kauli ya waumini wanapoitwa kwa Allaah na Mtume wake ili awahakumu kati yao, basi husema: “Tumesikia na tumetii” – na hao ndio wenye kufaulu. Na yeyote yule atakayemtii Allaah na Mtume wake na akamuogopa Allaah na akamcha, basi hao ndio wenye kufuzu.”[10]

Dameski

13 Jumaadaa al-Aakhirah 130

[1] 56:13-14

[2] Ibn ´Aabidiyn katika ”al-Haashiyah” (1/62). al-Luknawiy ameinasibisha kwa l-Ghazaaliy katika ”an-Naafi´ al-Kabiyr”, uk. 93

[3] Amesema mwanzoni mwa “Mukhtaswar Fiqh-ish-Shaafi´iy:

“Nimefupiliza kitabu hiki kutokana na elimu ya Muhammad bin Idriys ash-Shaafi´iy (Rahimahu Allaah) na kuchambua maneno yake, kwa ajili ya kumfanyia wepesi yule anayetaka kuisoma. Aidha mtu anatakiwa kujua kwamba amekataza kumfuata kichwa mchunga yeye na wengineo. Alikuwa anataka dini na nafsi ya mtu visalimike.”

[4] Amesema kwa uwazi kabisa kwamba anatofautiana na imamu wake katika masuala karibu ishirini. Yanapatikana 43, 44, 103, 120, 158, 169, 172, 173, 228, 230, 240, 244, 274, 275, 284, 314, 331, 338, 355 na 356. Tazama ”at-Ta´liyq al-Mumajjad ´alaa Muwattwa’ Muhammad”.

[5] al-Muwattwa’, uk. 158

[6] al-Faw-aaid al-Bahiyyah fiy Taraajim-il-Hanafiyyah, uk. 116

[7] al-Bahr ar-Raa-iq (6/93) na Rasm-ul-Muftiy (1/28).

[8] al-Fawaa-id, uk. 116. Taaliki yake ni nzuri:

“Hapa mtu anapata kujua kwamba upokezi wa Mak-huul kutoka kwa Abu Haniyfah ni batili, nayo inasema:

“Mwenye kunyanyua mikono yake pindi anaswali swalah yake inaharibika.”

Aamir Kaatib al-Atqaaniy ameghurika nayo, kama ilivyotajwa katika wasifu wake. ´Iswaam bin Yuusuf al-Balkhiy, ambaye alikuwa ni mwanafunzi wa Abu Yuusuf, alikuwa akinyanyua mikono yake. Lau upokezi huo ungelikuwa na msingi, basi ni jambo angelijua Abu Yuusuf na ´Iswaam.”

Amesema vilevile:

“Hanafiy anatakiwa kutambua kwamba endapo ataacha maoni ya imamu wake katika masuala fulani kwa sababu maoni mengine ndio yenye dalili ilio na nguvu zaidi, haina maana kwamba ametoka nje ya madhehebu. Yeye yumo ndani ya madhehebu. Huoni kuwa ´Iswaam bin Yuusuf aliyaacha maoni ya Abu Haniyfah kuhusu kunyanyua mikono na pamoja na hivyo bado anazingatiwa kuwa ni katika Hanafiyyah?”

Amesema tena:

“Allaah ndiye mwenye kufaa kushtakiwa kutokana na wajinga wa zama zetu. Wanamtukana yule mwenye kuacha kumfuata imamu wake kibubusa katika suala moja kwa sababu tu dalili nyingine ina nguvu zaidi na wanamtoa nje ya madhehebu. Si jambo la ajabu kwao, kwani ni katika ´Awwaam. Ajabu iko kwa wale wanaojifananisha na wanachuoni na wanatembea kama wao, kama wanyama.”

[9] 04:65

[10] 24:51-52

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 50-52
  • Imechapishwa: 21/01/2019