11. Umoja wa waislamu haukamiliki pasi na kumtii mtawala

Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimhu Allaah) amesema:

Msingi wa tatu:

Miongoni mwa utimilifu wa umoja ni usikivu na utiifu kwa yule ambaye amekuwa kiongozi juu yetu hata kama atakuwa ni mtumwa wa kihabeshi. Allaah amebainisha haya ubainifu wenye kutosheleza kwa njia mbalimbali miongoni mwa aina za ubainifu Kishari´ah na kwa Qadar.

Kisha ikawa msingi huu haujulikana kwa wengi wenye kudai elimu. Vipi basi wataufanyia kazi?

MAELEZO

Miongoni mwa utimilifu… – Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) ametaja kwamba miongoni mwa ukamilifu wa umoja ni kuwasikiliza na kuwatii watawala kwa kutekeleza yale waliyoamrisha na kuacha yale waliyokataza, ingawa yule anayetutawala ni mja wa kihabeshi.

Allaah amebainisha haya… – Kuhusu ubainifu Wake wa Kishari´ah ni ndani ya Qur-aan na Sunnah. Miongoni mwa ubainifu Wake ndani ya Qur-aan ni maneno Yake (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ

”Enyi mlioamini! Mtiini Allaah na mtiini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi.”[1]

 يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ

“Enyi walioamini! Mtiini Allaah na mtiini Mtume.”[2]

وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّـهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا

“Shikamaneni kwa kamba ya Allaah nyote pamoja wala msifarikiane.”[3]

Miongoni mwa ubainifu wake katika Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa salam) ni yale yaliyothibiti kwa al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa ´Ubaadah bin as-Swaamitw (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesema:

“Tulikula kiapo cha usikivu kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa salam) juu ya kusikiza na kutii, katika uchangamfu wetu na yale tunayoyachukia, katika kipindi chepesi na kigumu, pindi mtu anapopendelewa juu yetu na kwamba tusivutane na watawala mpaka pale mtakapoona ukafiri wa wazi ambao tuna dalili kwao kutoka kwa Allaah.”[4]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa salam):

“Ambaye ataona kutoka kwa kiongozi wake kitu basi asubiri. Kwani hakika yule atakayetengana na mkusanyiko kiasi cha shibiri akafa basi amekufa kifo cha kipindi cha kikafiri.”[5]

“Yule ambaye atajiondoa kutoka katika utiifu basi atakutana na Allaah siku ya Qiyaamah akiwa hana hoja.”[6]

“Sikiliza na utii ijapo utatawaliwa na mja muhabeshi.”[7]

“Ni lazima kwa mtu muislamu kusikiliza na kutii katika yale anayoyapenda na kuyachukia muda wa kuwa hajaamrishwa maasi. Akiamrishwa maasi basi hakuna utiifu kwa kiumbe katika kumuasi Muumba.”[8]

Kuna maafikiano juu yake.

´Abdullaah bin ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Tulikuwa pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika moja ya safari ambapo tukatua sehemu fulani. Tahamaki akaita mwitaji wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa kusema “Swalah ya pamoja.” Basi tukakusanyika mbele ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akasema:

“Hakika hakuna Mtume yeyote aliyetumilizwa na Allaah isipokuwa ilikuwa ni haki juu yake kuwajulisha watu wake katika ile kheri anayoyajua juu yao na kuwaonya ile shari anayoijua juu yao. Hakika ummah wenu huu umefanywa ustawi wake mwanzoni mwake na mwishoni mwake utafikwa na majanga na mambo wanayoyachukia; itakuja fitina hali ya kuwa iliotangulia itakuwa sahali kuliko inayofuata. Itakuja fitina ambapo muumini aseme: “Hii ni yenye kuangamiza.” Itakuja fitina nyingine aseme: “Hii sasa, hii sasa.” Yeyote anayetaka kuepukwa na Moto na kuingizwa Peponi basi kimjie kifo chake hali ya kuwa ni mwenye kumwamini Allaah na siku ya Mwisho na pia atangamane na watu vile anavyopenda kufanyiwa. Yule anayekula kiapo cha usikivu kwa kiongozi kwa mkono wake na kwa moyo wake wote basi amtii kadri na awezavyo. Akija mwingine kutaka kumng´oa basi kateni shingoni ya huyo mwingine.”[9]

Ameipokea Muslim.

[1] 04:59

[2] 04:59

[3] 03:103

[4] al-Bukhaariy (7056) na Muslim (1709).

[5] al-Bukhaariy (7054) na Muslim (1849).

[6] Muslim (1851).

[7] al-Bukhaariy (7142).

[8] al-Bukhaariy (7144) na Muslim (1839).

[9] Muslim (1844).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sittah, uk. 17-20
  • Imechapishwa: 21/06/2021