11. Uchambuzi wa udhaifu wa Hadiyth ya Mu´aadh bin Jabal

Kabla sijamaliza maneno yangu haya naonelea kuwa ni lazima kwangu kuwazindua ndugu waliohudhuria juu ya Hadiyth inayotambulika. Hadiyth hiyo inapatikana katika vitabu vya “Usuwl-ul-Fiqh” vyote na ni dhaifu inapokuja katika mlolongo wa wapokezi wake na pia inapingana na yale tumeyotoka kusoma katika kijitabu hiki ambapo haifai kutofautisha wakati wa kuweka Shari´ah kati ya Qur-aan na Sunnah na kwamba ni wajibu kuvitendea kazi vyote viwili kwa pamoja. Hadiyth hiyo si nyingine ni ile ya Mu´aadh bin Jabal (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kumwambia pindi alipomtuma kwenda Yemen:

“Utahukumu kwa nini?” Akasema: “Kwa Kitabu cha Allaah.” Akamwambia: “Usipopata?” Akasema: “Kwa Sunnah ya Mtume wa Allaah.” Akamwambia: “Usipopata?” Akasema: “Nitajitahidi rai yangu na wala sintovuka mipaka.” Akasema: “Himdi zote njema ni za Allaah ambaye amemuwafikisha mjumbe wa Mtume wa Allaah kwa yale anayoyapenda Mtume wa Allaah.”

Kuhusu udhaifu wa mlolongo wa wapokezi wake hakuna nafasi ya kuutaja kwa sasa. Nimebainisha hayo ubainifu wa kutosha, jambo ambalo sikutangulia kulifanya katika mifululizo uliotangulia kutajwa. Hivi sasa nitatosheka na kutaja ya kwamba kiongozi wa waumini katika Hadiyth ambaye ni Imaam al-Bukhaariy (Rahimahu Allaah) amesema juu yake:

“Hadiyth ni yenye kukataliwa.”

Baada ya haya inafaa kwangu kuanza kutaja ule mgongano niliyouashiria kwa kusema:

al-Haakim ameweka mfumo akitegemea Hadiyth hii ya Mu´aadh juu ya kuhukumu katika ngazi tatu ambapo haijuzu kutafuta hukumu katika maoni isipokuwa baada ya mtu kukosa katika Sunnah kama ambavyo vilevile haijuzu kwa mtu kutafuta katika Sunnah isipokuwa baada ya kukosa katika Qur-aan. Kwa mujibu wa wanachuoni wote huu ni mfumo sahihi inapokuja katika maoni. Wanachuoni vilevile wamesema kwamba kunapothibiti upokezi basi maoni hayana nafasi. Lakini hata hivyo inapokuja katika Sunnah sio sahihi, kwa kuwa Sunnah ndio inayoihukumu Qur-aan na kuibainisha. Kwa hivyo ni wajibu kutafuta hukumu katika Sunnah hata kama mtu anaweza kufikiria kuwa inapatikana katika Qur-aan. Haya ni kutokana na yale tuliyosema kuwa mafungamano ya Sunnah kwa Qur-aan sio kama maoni kwa Sunnah. Hapana sivyo hivyo kabisa. Bali ni wajibu kuizingatia Qur-aan na Sunnah kama chanzo kimoja na kwamba haviwezi hata siku moja kutenganishwa, kama yalivyoashiria maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Tanabahini! Hakika mimi nimepewa Qur-aan na mfano wake pamoja.”

Bi maana Sunnah.

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Havitotengana mpaka nijiwe katika hodhi.”

Migawanyo iliyotajwa ni jambo ambalo si sahihi, kwa kuwa inapelekea kuvigawanya kati yake. Hili ni jambo la batili kutokana na yale tuliyotangulia kuyataja. Haya ndio yale niliyotaka kuyabainisha. Iwapo nimepatia, basi yanatokamana na Allaah, endapo nimekosea, basi yanatokamana na nafsi yangu.

Ninamuomba Allaah atukinge sote kutokamana na kuteleza na kutokamana na yale yote asiyoyaridhia. Maombi yetu ya mwisho ni: Himdi zote njema anastahiki Allaah, Mola wa walimwengu.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Manzilat-us-Sunnah fiyl-Islaam, uk. 20-23
  • Imechapishwa: 10/02/2017