11. Sharti ya nane ya swalah


Shaykh-ul-Islaam na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Sharti ya nane ni kuelekea Qiblah. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

قَدْ نَرَى تَقَلُّبَ وَجْهِكَ فِي السَّمَاء فَلَنُوَلِّيَنَّكَ قِبْلَةً تَرْضَاهَا فَوَلِّ وَجْهَكَ شَطْرَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ وَحَيْثُ مَا كُنتُمْ فَوَلُّواْ وُجُوِهَكُمْ شَطْرَهُ

“Hakika Tumeona unavyogeuzageuza uso wako mbinguni, basi Tutakuelekeza Qiblah kinachokuridhisha. Hivyo basi uelekeze uso wako upande wa Msikiti mtakatifu; na popote mtakapokuwepo basi zielekezeni nyuso zenu upande wake.”[1]

MAELEZO

Kuelekea Qiblah ambapo ni Ka´bah. Ni lazima kwa mtu kukielekea katika swalah za faradhi na za sunnah. Dalili ya hilo ni Aayah tukufu. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

قَدْ نَرَى تَقَلُّبَ وَجْهِكَ فِي السَّمَاء فَلَنُوَلِّيَنَّكَ قِبْلَةً تَرْضَاهَا فَوَلِّ وَجْهَكَ شَطْرَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ وَحَيْثُ مَا كُنتُمْ فَوَلُّواْ وُجُوِهَكُمْ شَطْرَهُ

“Hakika Tumeona unavyogeuzageuza uso wako mbinguni, basi Tutakuelekeza Qiblah kinachokuridhisha. Hivyo basi uelekeze uso wako upande wa Msikiti mtakatifu; na popote mtakapokuwepo basi zielekezeni nyuso zenu upande wake.”

Hata hivyo hakuna neno kuelekea upande mwingine kukiwa kuna udhuru wa Kishari´ah. Mfano wa udhuru huo ni kama msafiri anayeswali swalah ya sunnah wakati wa safari yake. Inajuzu kwa sababu hilo lina udhuru wa Kishari´ah. Udhuru mwingine ni kama mgonjwa ambaye hawezi kuelekea Qiblah na anachelea wakati usije kutoka nje. Basi aswali kadiri anavoweza:

فَاتَّقُوا اللَّـهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ

”Mcheni Allaah muwezavyo.”[2]

Mtu ni mgonjwa ameshindwa kuelekea Qiblah na hakuna awezaye kumwelekeza Qiblah. Hakuna neno. Mfano mwingine ni mfungwa ambaye amefungwa au amesulubiwa na hana uwezo wa kuelekea Qiblah. Katika hali hii Allaah (Jalla wa ´Alaa) anasema:

فَاتَّقُوا اللَّـهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ

”Mcheni Allaah muwezavyo.”

لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا

”Allaah hakalifishi nafsi yoyote isipokuwa kwa kadiri ya uwezo wake.”[3]

Ama mtu akiwa na uwezo ni lazima aelekee Qiblah, ni mamoja katika swalah za faradhi au za sunnah. Isipokuwa katika safari. Wakati wa safari hakuna neno akaswali swalah za sunnah katika upande mwingine.

[1] 02:144

[2] 64:16

[3] 02:286

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ash-Sharh al-Mumtaaz, uk. 83
  • Imechapishwa: 30/06/2018