11. Safari kwa ajili ya kutembelea kaburi la Mtume

Swali: Ni ipi hukumu ya kuanzisha safari kwa ajili ya kutembelea kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)? Ni ipi njia iliowekwa katika Shari´ah ya kulitembelea kaburi lake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)?

Jibu: Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kufunga safari isipokuwa kuiendea misikiti mitatu; msikiti Mtakatifu, msikiti wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na msikiti wa al-Aqswaa.

Hakufungwi safari kwa ajili ya kaburi lake. Lakini muislamu anamswalia na kumtakia amani kila mahali. Hapana haja ya kufunga safari kumwendea. Una uwezo wa kumswalia na kumtakia amani na wewe uko nyumbani kwako, uko ndani ya ndege, ndani ya gari. Allaah amerahisisha jambo hilo. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Niswalieni. Kwani hakika swalah zenu zinanifikia popote mnapokuwa.”[1]

Jambo limewepesishwa. Kuna haja gani ya kufunga safari? Anayemswalia mara moja basi Allaah anamsifu mara kumi. Anayemtakia amani mara moja basi Allaah anamtakia amani mara kumi.

Unaweza kumswalia ukitembelea Madiynah kwa ajili ya kuswali ndani ya msikiti. Kipindi hicho kulitembelea kaburi kunafuatia kuutembelea msikiti. Kwa hivyo usitegemeze wala kufunga safarikwa ajili ya kaburi. Kunafungwa safari kwa ajili ya kuutembelea msikiti na kaburi litafuatia jambo hilo. Kwa kumalizia ni kwamba safari haifungwi isipokuwa kwa ajili ya misikiti hii mitatu peke yake. Wala safari haifungwi kwa ajili ya kaburi miongoni mwa makaburi kabisa hata kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Lakini safari inafungwa kwa sababu ya kuuendea msikiti peke yake. Kaburi halipo ndani ya msikiti. Kaburi lipo nyumbani kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhumaa).

[1] Ahmad (8586).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tahdhiyr min Fitnat-il-Qubuur, uk. 53-54
  • Imechapishwa: 21/04/2022