[15] Baada ya kumaliza kisomo na kabla ya kwenda katika Rukuu´, wakati mwingine alikuwa akisoma du´aa ya Qunuut ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimfunza mjukuu wake al-Hasan bin ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anhumaa):

اللهم اهدني فيمن هديت, وعافني فيمن عافيت, وتولني فيمن توليت, وبارك لي فيما أعطيت, وقني شر ما قضيت, فإنك تقضي ولا يقضى عليك, وإنه لا يذلّ من واليتَ, ولا يعزّ من عاديت, تباركت ربنا وتعاليت، لا منجا منك إلا إليك

“Ee Allaah! Niongoze pamoja na wale Uliowaongoza, uniafu pamoja na wale Uliowaafu, Uniangalie pamoja na wale Unaowaangalia, Unibariki katika kile Ulichotoa na Unilinde kutokamana na shari kwa yale Uliyohukumu. Kwani hakika Wewe ndiye mwenye kuhukumu na wala Huhukumiwi. Hakika hatwezeki yule Uliyemfanya mpenzi na wala hapati nguvu yule Uliyemfanya adui. Umebarikika na Umetukuka Mola wetu. Hakuna mahali pa kuokoka kutokamana na Wewe isipokuwa Kwako.”[1]

Baada ya hapo ni sawa wakati fulani kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[16] Hakuna neno kwa yule atakayesoma Qunuut baada ya Rukuu´ na kama nyongeza akawalaani makafiri, akamswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akawaombea du´aa waislamu katika ile nusu ya pili ya Ramadhaan. Imethibiti kuwa maimamu kipindi cha ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) walifanya hivo. Imekuja mwishoni mwa Hadiyth ya ´Abdur-Rahmaan bin ´Abd al-Qaariy:

“Walikuwa wakiwalaani makafiri baada ya nusu [ya mwezi]: “Ee Allaah! Wapige vita makafiri ambao wanazuilia na njia Yako, wanawakadhibisha Mitume Wako na wala hawaamini ahadi Yako. Watofautishe, tia woga ndani ya mioyo yao na ufanye utwevu na adhabu Yako viwapate – Ee Mungu wa haki!” Halafu wanamswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wanawaombea kheri waislamu na msamaha waumini. Kisha wanasema: “Ee Allaah! Hakika Wewe ndiye tunakuabudu, Kwako Wewe tu ndiye tunaswali na kusujudu na Kwako ndiko tunakimbilia. Tunataraji huruma Yako, ee Mola wetu, na tunakhofu adhabu Yako ya kisawasawa. Hakika adhabu Yako itawapata wale ambao ni adui Zako.” Kisha mtu analeta Takbiyr na kusujudu.”[2]

[1] Ameipokea Abu Daawuud, an-Nasaa´iy na wengineo. Mlolongo wa wapokezi ni Swahiyh. Tazama “Swifat-us-Swalaah”, uk. 95-96, chapisho la saba.

[2] Ameipokea Ibn Khuzaymah katika “as-Swahiyh” yake (02/155-156/1100).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qiyaam Ramadhwaan, uk. 31-32
  • Imechapishwa: 07/05/2019