11. Pokea zawadi ya ndugu yako


38- Muslim amepokea kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimpa zawadi ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) ambapo ´Umar akawa amemwambia:

“Mpe mwingine aliye fakiri kuliko mimi.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia: “Ichukue utaipeana au uitoe swadaqah. Mali inayokujia pasina wewe kuipupia au kuiomba unatakiwa kuipokea. La sivyo iache.”[1]

39- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ukipata kitu pasina kukiomba kile na utoe swadaqah.”[2]

40- Khaalid bin ´Adiyy al-Juhaniy ameeleza kuwa amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Yule miongoni mwenu mwenye kupata kitu kutoka kwa ndugu yake pasina kukiomba au kukipupia akipokee na asikirudishe. Ni riziki ambayo Allaah amemruzuku.”[3]

41- Mlango huu usifahamike dhahiri yake au pasina kufungamana, kama jinsi wanavofanya baadhi ya mafukara na wajinga. Haijuzu kupokea kitu ambacho ni haramu. Ni wajibu kukirudisha. Mfano wa hilo ni pesa kutoka kwa mtawala dhalimu au mtu mwenye kazi ya haramu kama mpiga ngoma, mtengenezaji ala za muziki, mmiliki wa baa, watu wa ushuru, wakusanyaji wa asilimia kumi, mwimbaji, wakodeshwaji wa kulia na wengine. Kwa sababu kazi zao ni haramu kwa maafikiano.

42- Ibn ´Abdil-Barr amesema:

“Miongoni mwa mapato ambayo kuna maafikiano juu ya uharamu wake ni ribaa, kipato cha malaya, pesa ya haramu, rushwa, malipo kwa ajili ya maombolezo, nyimbo, uganga, urozi, michezo ya alama za muziki, michezo na vitu vinginevyo vyote vya kipuuzi.

43- Chumo lingine ambalo kuna maafikiano vilevile juu ya uharamu wake ni lile la kuchukua kwa nguvu, wizi na kila chenye kuchukuliwa pasina kupenda kwa mmiliki. Haijalishi kitu sawa mmiliki akiwa ni muislamu au Dhimmiy.

44- Wanachuoni wengine wanasema kuwa mali ikichanganyika na kitu katika halali, hilo ni jambo la nadra kutokea na nadra haina hukumu yoyote. Kadhalika hushindwa kuonekana ni kipi cha halali katika mali hii kwa sababu kwa kiasi kikubwa huwa ni haramu. Mwenye kupokea zawadi ya mwenye kufanya dhuluma anamsaidia katika dhuluma. Kuna khatari pia akaanza kumpenda na yeye akaanza kumuasi Allaah (Ta´ala).

45- Sufyaan ath-Thawriy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Mwenye kupokea mali au silaha kutoka kwa mtu dhalimu na akapambana kwavyo katika njia ya Allaah analaaniwa kwa kila siku anapovichukua na kuviweka chini mpaka ataporejea.”

46- Sufyaan ath-Thawriy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Mwenye kumuombea dhalimu maisha marefu basi anataka Allaah (´Azza wa Jall) aasiwe.”

[1] al-Bukhaariy (1473) na Muslim (1045).

[2] Muslim (1045).

[3] Ahmad (4/220). Swahiyh kwa mujibu wa al-Haythamiy katika ”Majma´-uz-Zawaa-id” (3/100).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Ahmad al-Qurtwubiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qam´-ul-Hirsw biz-Zuhd wal-Qanaa´ah, uk. 42-44
  • Imechapishwa: 18/03/2017