11. Mukhtasari wa mlango wa 36

Maandiko haya ya Qur-aan na ya Sunnah yanafahamisha juu ya mambo makubwa:

1- Aayah zinafahamisha kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) si vyengine isipokuwa ni mtu tu. Hana uola wala uungu wowote. Ndani yake kuna Radd kwa wale wanaochupa mipaka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), wanaamini kuwa ana sifa fulani ya uola na wanamwita na kumuomba msaada yeye na haja mbalimbali badala ya Allaah, jambo ambalo ni shirki kubwa.

2- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametumilizwa kwa ajili ya kulingania katika Tawhiyd na kumshirikisha Allaah (´Azza wa Jall). Mitume na Manabii wengine walikuwa na jukumu hilohilo. Hii ndio kazi na jukumu kubwa zaidi.

3- Ulazima wa kumtakasia matendo Allaah (´Azza wa Jall). Hili ndio jambo kusudiwa la mlango.

4- Katika Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) kuna dalili inayoonyesha kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) hana haja ya ´ibaadah za waja. Lau viumbe wote wangeshirikisha au wakakufuru basi hayo yasingepunguza kitu katika ufalme Wake.

5- Katika Hadiyth hiyohiyo kuna matahadharisho juu ya shirki katika matendo. Shirki inasababisha kitendo kurudishwa na kutokukubaliwa, ni mamoja kitendo hicho kimechanganyika na shirki kubwa au ndogo ikiwa ni pamoja na kujionyesha.

6- Allaah (Jalla wa ´Alaa) anazungumza vile anavotaka. Maneno ni moja katika sifa Zake (Subhaanah). Ni moja katika sifa za kimatendo ambazo zinalingana na utukufu Wake. Sio kama maneno ya viumbe. Ni maneno yanayolingana na utukufu Wake (Subhaanahu wa Ta´ala).

7- Katika Hadiyth ya Abu Sa´iyd (Radhiya Allaahu ´anh) kuna matahadharisho juu ya shirki na ubainifu wa maana yake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameifasiri pale aliposema:

“Ni shirki iliyojificha; anasimama mtu kuswali na akaipamba swalah yake kwa kuwa anaona watu wanamwangalia.”

8- Katika Hadiyth hiyohiyo kuna dalili inayoonyesha kuwa shirki imegawanyika kunako shirki ya waziazi na shirki iliyojificha. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ni shirki iliyojificha… “

Ina maana kwamba pia kuna shirki ya wazi. Ni shirki inayokuwa katika matendo yenye kuonekana kama mfano wa Rukuu´, Sujuud, du´aa, kuchinja na nadhiri. Anapofanyiwa ´ibaadah hizi mwengine asiyekuwa Allaah inakuwa shirki ya waziwazi.

Kujionyesha ni shirki iliyojificha. Inakuwa kwenye mioyo na makusudio. Kwa ajili hii imekuja katika Hadiyth:

“Shirki katika Ummah huu imejificha kuliko mdudumchungu mweusi juu ya jiwe jeusi katika usiku wenye giza. Kafara yake ni kusema:

اللهم إني أعوذُ بك أن أشرِكَ بك و أنا أعلمُ ، و أستغفِرُك لما لا أَعلمُ

“Ee Allaah! Najilinda Kwako kukushirikisha Wewe ilihali najua na Unisamehe kwa yale nisiyoyajua.“[1]

Maswahabah walikuwa wakiiogopa shirki hii. Kila ambavyo imani ya mtu inakuwa na nguvu zaidi ndivo kuogopa kwake kujionyesha na shirki zengine zote kunakuwa kukubwa zaidi.

[1] Ahmad (1906). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh al-Adab al-Mufrad” (551).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: I´aanat-ul-Mustafiyd bi Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 446-447
  • Imechapishwa: 24/07/2019