11. Mtazamo wa Ahl-us-Sunnah kwa Maswahabah wa Mtume wa Allaah

Katika kumuamini Allaah kunaingia vilevile kupenda na kuchukia kwa ajili ya Allaah na kujenga urafiki na uadui kwa ajili ya Allaah. Muumini anatakiwa kuwapenda waumini na kujenga nao urafiki na anatakiwa vilevile kuwachukia makafiri na kujenga uadui kwao. Waumini wanaochukua nafasi ya mbele katika ummah huu ni Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa hiyo Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanawapenda na kujenga nao urafiki na vilevile wanaonelea kuwa wao ndio watu bora baada ya Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watu bora ni wa karne yangu. Kisha wataofuatia. Kisha wataofuatia.”[1]

Kuna maafikiano juu ya usahihi wake.

Wanaitakidi kuwa mbora wao ni Abu Bakr asw-Swiddiyq, halafu ´Umar al-Faaruq, halafu ´Uthmaan Dhun-Nuurayn kisha ´Aliy al-Murtadhwaa (Radhiya Allaahu ´anhum).

Baada yao wanaofuata ni wale Maswahabah kumi wengine waliobaki halafu Maswahabah wengine waliobaki (Radhiya Allaahu ´anhum).

Wananyamazia yale yote yaliyopitika kati ya Maswahabah na wakati huohuo wanaonelea kuwa katika hayo walikuwa ni wenye kufanya Ijtihaad. Aliyepatia, basi ana ujira mara mbili, na aliyekosea ana ujira mara moja.

Vilevile wanawapenda watu wa familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) waliomuamini na wanajenga urafiki nao na wakeze Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambao ndio mama wa waumini, na wanawatakia radhi wote kwa pamoja.

Ahl-us-Sunnah ni wenye kujitenga mbali kabisa na mfumo wa Raafidhwah ambao wanawachukia Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kuwatukana na sambamba na hilo wanapetuka mipaka kwa watu wa familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wanawanyanyua zaidi ya nafasi zao walizopewa na Allaah. Ahl-us-Sunnah vilevile wanajitenga mbali kabisa na mfumo wa Nawaaswib ambao wanawaudhi watu wa familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aidha kwa maneno au vitendo.

Yale yote tuliyoyataja katika maneno haya machache yanaingia katika ´Aqiydah sahihi ambayo Allaah amemtuma nayo Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hiyo ndio ´Aqiydah ya kundi lililookoka, Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah, ambao Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema juu yao:

“Hakitoacha kikundi katika ummah wangu kuwa juu ya haki hali ya kuwa ni chenye kunusuriwa. Hakitodhurika na wale wenye kuwakosesha nusura mpaka ifike amri ya Allaah (Subhaanah).”[2]

“Mayahudi wamefarikiana mapote sabini na moja na wakristo wamefarikiana mapote sabini na mbili. Ummah huu utakuja kufarikiana mapote sabini na tatu. Yote yataingia Motoni isipokuwa moja tu.” Maswahabah wakauliza: “Ni lipi hilo, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: “Ni wale wataokuwa juu ya yale niliyomo mimi hii leo na Maswahabah wangu.””[3]

Nayo si mengine ni ile ´Aqiydah ambayo ni wajibu kuiamini, kuwa na msimamo juu yake na kutahadhari na yale yanayoenda kinyume nayo.

[1] al-Bukhaariy (2509), Muslim (2533), at-Tirmidhiy (3859), Ibn Maajah (2362) na Ahmad (01/434).

[2] Muslim (1920), at-Tirmidhiy (2229), Abu Daawuud (4252), Ibn Maajah (3952) na Ahmad (05/279).

[3] Ibn Maajah (3992).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Aqiydah as-Swahiyhah wa maa yudhwaadduhaa, uk. 11
  • Imechapishwa: 30/05/2023