Miongoni mwa misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni kuwa imani ni maneno, matendo na kuamini na kwamba inazidi kwa utiifu na inapungua kwa maasi. Imani sio maneno na vitendo pasi na kuamini, kwa sababu hii ni imani ya wanafiki, kama ambavo imani sio kule kutambua peke yake pasi na maneno na vitendo, kwa kuwa hii ni imani ya makafiri wakanushaji. Amesema (Ta´ala):

وَجَحَدُوا بِهَا وَاسْتَيْقَنَتْهَا أَنفُسُهُمْ ظُلْمًا وَعُلُوًّا

“Wakazikanusha na hali kuwa nafsi zao zimeziyakinisha kwa dhulma na majivuno.”[1]

فَإِنَّهُمْ لَا يُكَذِّبُونَكَ وَلَـٰكِنَّ الظَّالِمِينَ بِآيَاتِ اللَّـهِ يَجْحَدُونَ

“Basi hakika wao hawakukadhibishi wewe, lakini madhalimu wanakanusha Aayah za Allaah.”[2]

وَعَادًا وَثَمُودَ وَقَد تَّبَيَّنَ لَكُم مِّن مَّسَاكِنِهِمْ ۖ وَزَيَّنَ لَهُمُ الشَّيْطَانُ أَعْمَالَهُمْ فَصَدَّهُمْ عَنِ السَّبِيلِ وَكَانُوا مُسْتَبْصِرِينَ

“Kina ‘Aad na Thamuud na yamekwishakubainikieni masikani yao na shaytwaan aliwapambia matendo yao akawazuia na njia na walikuwa ni wenye kutambua vizuri.”[3]

Vilevile imani sio kule kuamini peke yake au kuzungumza na kuamini peke yake pasi na vitendo, kwa sababu hii ni imani ya Murji-ah. Allaah (Ta´ala) mara nyingi ameita vitendo kuwa ni “imani.” Amesema (Ta´ala):

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللَّـهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَانًا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ الَّذِينَ يُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُؤْمِنُونَ حَقًّا

“Hakika si venginevyo waumini ni wale ambao anapotajwa Allaah nyoyo zao zinajaa khofu na wanaposomewa Aayah Zake huwazidishia imani na kwa Mola wao wanategemea – ambao wanasimamisha swalah na hutoa sehemu katika yale Tuliyowaruzuku. Hao ndio waumini wa kweli!”[4]

وَمَا كَانَ اللَّـهُ لِيُضِيعَ إِيمَانَكُمْ

“Allaah hakuwa mwenye kupoteza imani zenu.”[5]

Bi maana swalah zenu mlizoswali kuelekea Jerusalemu. Hivyo akawa ameita swalah kuwa ni “imani.”

[1] 27:14

[2] 06:33

[3] 29:38

[4] 08:02-04

[5] 02:143

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Min Usuwl ´Aqiydah Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 22-24
  • Imechapishwa: 12/05/2022