11. Mfumo wa Salafiyyah uko wazi


Sote tunataka mabustani haya ambayo chini yake kunapita mito. Sote hatutaki Moto wala adhabu. Lakini tunachokiongelea hapa ni kufanya zile sababu zitazotufikisha Peponi na kutuokoa na Moto. Hakuna sababu zaidi ya kulazimiana na mfumo wa Salaf-us-Swaalih. Imaam Maalik (Rahimahu Allaah) amesema:

“Hautofaulu mwisho wa Ummah huu isipokuwa kwa waliofaulu kwayo wa mwanzo wao.”

Watu wa mwanzo walifaulu kwa kitu gani? Qur-aan na Sunnah. Vivyo hivyo hautofaulu mwisho wa Ummah huu isipokuwa kwa Qur-aan na Sunnah. Na Qur-aan na Sunnah vipo mbele yetu. Vimehifadhiwa na hifadhi ya Allaah:

إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا الذِّكْرَ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ

“Hakika Sisi ndio tulioteremsha Ukumbusho na hakika Sisi ndio tutaolinda.” (15:09)

Umelindwa kwa idhini ya Allaah. Mwenye kutaka haki na elimu sahihi atapata haya. Kuhusiana na mwenye kudai pasi na uhakika au anafuata kichwa mchunga wale wenye kudai Salafiyyah ilihali hawafuati mfumo wa Salaf haisaidii kitu. Tatizo ni kuwa wanayofanya watu hawa wanayanasibisha na Salafiyyah na Salafiyyuun, jambo ambalo ni kuwazulia uongo Salaf na Salafiyyah. Huku ni kukimbiza watu, sawa ikiwa kakusudia kufanya hivi au hakukusudia. Anayefanya hivi ima ni jitu linalofuata matamanio yake au ni mtu mjinga. Madai yasiyosimamishiwa dalili hubaki ni madai matupu. Ni lazima kwa yule mwenye kudai na kujinasibisha na Salaf ahakikishe jina hili na unasibisho huu. Hilo litapatikana kwa yeye kuonekane kwake kikweli mfumo wa Salaf; sawa inapokuja katika ´Aqiydah yake, maneno yake, matendo yake na matangamano yake mpaka awe Salafiy wa haki na awe ni kiigizo bora. Anachotakiwa ni kuwakilisha mfumo wa Salaf.

Mwenye kutaka mfumo huu ni juu yake kujifunza nao, kuusoma, kuufanyia kazi juu ya nafsi yake kwanza, alinganie watu kwao na awabainishie watu. Kwani hii ndio njia ya uokovu na hii ndio njia ya Firqat-un-Naajiyah; Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Ni wale wenye kufuata yale aliyokuwa akifuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah wake, astahamili kwa hilo na awe thabiti kwa hilo. Asikumbwe na fitina na madai potofu. Bali abaki kuwa imara katika yale aliyomo mpaka pale atapokutana na Mola Wake (Subhaanahu wa Ta´ala).

Allaah atuongoze sote katika yale anayoyapenda na kuyaridhia. Swalah na salaam zimwendee Mtume wetu Muhammad, ahli zake na Maswahabah zake wote.