11. Makadirio ya Allaah hayatakiwi kuhojiwa

Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

Kuamini Qadar ni moja katika zile nguzo sita za imani; yule mwenye kuipinga amekufuru. Yule mwenye kuipinga na akakinzana nayo ameikadhibisha Qur-aan. Yule mwenye kuikadhibisha Qur-aan amekufuru ukafiri mkubwa unaomtoa nje ya Uislamu.

Tumeshatangulia huko mbele ya kwamba Qadar ambao wanakanusha Qadar ni kipote kilichopotea na kinachopoteza. Wanaamini kwamba hakuna Qadar na kwamba Allaah hayajui mambo isipokuwa baada ya kutokea kwake. Kipote hicho kilianzishwa na Ma´bad al-Juhaniy na Ghaylaan ad-Dimashqiy. Kilienea mwishoni mwa zama za Maswahabah. Wakati ´Abdullaah bin ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anhumaa) alipopata khabari zao akajitenga nao mbali na kutokamana na I´tiqaad zao mbovu.

Hii leo kunapitika maneno ya khatari kwenye midomo ya watu wasiokuwa na elimu ambao wanasema kwamba Allaah anakadiria mazuri tu. Maana ya maneno haya ni kwamba Allaah hakadirii shari. Uhakika wa mambo ni kwamba kheri na shari vyote viwili vimekadiriwa. Allaah (Ta´ala) amesema:

كُلُّ نَفْسٍ ذَائِقَةُ الْمَوْتِ ۗ وَنَبْلُوكُم بِالشَّرِّ وَالْخَيْرِ فِتْنَةً

“Kila nafsi itaonja mauti na tutakujaribuni kwa mitihani ya shari na ya kheri.”[1]

Hivo ndivo wanavosema. Wamerithi msemo huu wenye ugonjwa. Ni lazima kwa wanafunzi kuwabainishia watu khatari yake na hiyo ina maana kwamba mtu mwenyewe ndiye anayejipangia shari. Hivo ndivo wanavosema Qadariyyah. ´Aqiydah hii ni batili kwa mujibu wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Allaah ametueleza kwamba Yeye anakadiria ya kheri na ya shari kwa sababu Yeye ni Mwenye nguvu sana, Mwenye hekima  na mjuzi wa kila jambo:

لَا يُسْأَلُ عَمَّا يَفْعَلُ وَهُمْ يُسْأَلُونَ

“Haulizwi [Allaah] kwa yale anayoyafanya, lakini wao wataulizwa.”[2]

Imekuja katika mapokezi:

“Lau Allaah angeliwaadhibu wakazi wa mbinguni na wakazi wa ardhini basi angeliwaadhibu pasi na kuwa ni mwenye kuwaadhibu. Na angeliwarehemu basi rehema Yake ingelikuwa yenye wasaa zaidi kuliko matendo yao.”[3]

Kwa hivyo hakuna chochote katika makadirio ya Allaah kinachofanyiwa upinzani. Mtu hatakiwi kuhoji ni kwa nini Allaah amemuumba shaytwaan au ni kwa nini Anataka kafiri akufuru au mtenda dhambi atende dhambi. Hakuna anayesema hivo isipokuwa aliye mjinga au mtu aliyepinda ambaye anaijua haki pasi na kuisaidikisha.

[1] 21:35

[2] 21:23

[3] Abu Daawuud (4699).

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 59-60
  • Imechapishwa: 03/10/2019