11. Madhehebu ya Khawaarij na sampuli za kufuru na shirki


Watu inapokuja katika vitenguzi hivi wamegawanyika mafungu matatu:

1- Kundi la kwanza: Ni wale wanaopetuka mipaka katika kukufurisha na kuwatia watu ukafirini. Wanapetuka mipaka katika kukufurisha na wanawakufurisha watu bila ya mapokezi, uelewa na maarifa. Haya ndio madhehebu ya Khawaarij ambao walijitokeza katika zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), katika zama za makhaliyfah waongofu na katika zama za nyuma. Hawa wanawakufurisha waislamu na wanapetuka mipaka kwa kutiana katika kufuru. Kila yule ambaye anakwenda kinyume nao wanamkufurisha na kuhalalisha damu yake. Khawaarij wana misingi ifuatayo:

Msingi wa kwanza: Kuwakufurisha watu kwa kutenda madhambi makubwa ambayo ni chini ya kufuru.

Msingi wa pili: Kutoka katika utiifu wa mtawala wa waislamu na kusambaratisha umoja wao.

Msingi wa tatu: Kuhalalisha damu ya waislamu.

Haya ni kwa sababu ya kutendea kazi maandiko yanayofahamisha, kwa udhahiri wake, juu ya kufuru au shirki. Wameyatendea kazi kwa uinje wake bila kuyaoanisha kati yake na maandiko mengine ambayo yanayafasiri na kuyaweka wazi zaidi.

Kwani hakika kufuru imegawanyika aina mbili:

Ya kwanza: Kufuru kubwa.

Ya pili: Kufuru ndogo.

Shirki pia imegawanyika aina mbili.

Ya kwanza: Shirki kubwa.

Ya pili: Shirki ndogo.

Shirki kubwa inamtoa mtu katika dini na inatengua Uislamu wa mtu.

Shirki ndogo haimtoi mtu katika dini. Lakini hata hivyo inaupunguza Uislamu na imani.

Wao – yaani Khawaarij – hawatofautishi baina ya haya mawili. Hawana kufuru ndogo wala shirki ndogo. Wanaonelea kuwa kufuru kwao ni kitu kimoja tu; zote mbili zinamtoa mtu katika dini. Vilevile wametendea kazi maandiko kwa uinje wake na wakaacha maandiko mengine ambayo yanapambanua mambo haya na kuyagawa mafungu mawili. Wamefanya hivi kutokana na kutokuwa kwao na ufahamu na uelewa wa dini na kutokomaa kwao kielimu. Matokeo yake wakawa wanawakufurisha watu hovyo hovyo tu na wakapindukia katika kukufurisha pasi na uelewa wala mategemezi. Wakawa wanayatendea kazi maandiko pasipo mahala pake. Yote haya kwa kuwa hawana uelewa zaidi ya kusoma tu. Wanasoma matamko na wala hawafahamu maana na hatimaye wanayatendea kazi watu.

Hawa ndio Khawaarij. Kwa masikitiko makubwa leo Khawaarij wana warithi katika wale wanaowakufurisha watu, kupetuka mipaka katika kukufurisha na kuhalalisha damu kwa hoja kwamba watu hawa ni makafiri. Wana warithi hii leo kutoka katika vijana wetu, wajinga wetu na wanaojifanya ni wasomi.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 24-26
  • Imechapishwa: 06/05/2018