Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya miti na mawe ni maneno Yake (Ta´ala):

أَفَرَأَيْتُمُ اللَّاتَ وَالْعُزَّىٰ وَمَنَاةَ الثَّالِثَةَ الْأُخْرَىٰ

“Je, mmeona al-Laat na al-‘Uzzaa na Manaat mwengine wa tatu?” (53:19-20)

MAELEZO

Aayah hii inathibitisha kwamba kuna washirikina wenye kuabudu mawe na miti.

Maneno yake Yake:

أَفَرَأَيْتُمُ اللَّاتَ

“Je, mmeona al-Laat… ”

ni swali kwa njia ya kukemea, likiwa na maana “Nijuzeni”, kwa njia ya swali la kukemea na kukifanya kibaya kitendo hicho.

al-Laat ilikuwa ni sanamu at-Twaaif ambalo lilikuwa ni jiwe lililozikwa. Ilikuwa ni jengo liliyojengwa sawa na Ka´bah. Ilikuwa limezungukwa na uwanja ulio na walinzi. Walikuwa wakiliabudu badala ya Allaah (´Azza wa Jall). Lilikuwa la Thaqiyf na washirika wao katika makabila mbalimbali ambao walikuwa wakijifakhari nalo.

al-Laat alikuwa ni mwanaume mwema aliyekuwa akipika uji na akiwapa mahujaji. Alipokufa, wakajenga jengo juu ya kaburi lake ambalo walilifunika kwa pazia. Hivyo wakawa wanaliabudu badala ya Allaah (´Azza wa Jall).

al-´Uzzaa ilikuwa ni miti mingi ya mtende kati ya Makkah na at-Twaaif. Pembezoni mwake kulikuwa jengo lililofunikwa likiwa na walinzi. Kulikuwa mashaytwaan yanayowazungumzisha watu. Wajinga walikuwa wakidhani kuwa miti na jengo ndio vinavyozungumza na wao. Ilikuwa ni mashaytwaan ndio wenye kuzungumza nao ili kuwapotosha na njia ya Allaah. Sanamu hili lilikuwa la Quraysh, watu wa Makkah na walioko pembezoni mwake.

Manaat ilikuwa ni jiwe kubwa lililokuwa karibu na mlima wa Qudayd kati ya Makkah na al-Madiynah. Lilikuwa ni la Khuzaa´ah, al-Aws na al-Khazraj. Walikuwa wakihirimia kutoka kwenye jiwe hilo wanapoelekea hajj na wanaliabudia badala ya Allaah. Haya ndio yalikuwa masanamu matatu makubwa ya waarabu. Allaah (Ta´ala) amesema:

أَفَرَأَيْتُمُ اللَّاتَ وَالْعُزَّىٰ وَمَنَاةَ الثَّالِثَةَ الْأُخْرَىٰ

“Je, mmeona al-Laat na al-‘Uzzaa na Manaat mwengine wa tatu?”

Je, yalikupeni faida yoyote? Yalikunufaisheni? Yalikuwa yakikunusuruni? Je, yalikuwa yakiumba, yakiruzuku, yakihuisha na yakifisha? Mlipata nini kwayo? Hili ni kwa njia ya kukemea na kuzizindua akili ziweze kurudi katika usawa wake. Vitu hivi si vyengine isipokuwa ni mawe na miti isiyonufaisha wala kudhuru.

Pindi Allaah alipoleta Uislamu na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaiteka Makkah, alimtuma al-Mughiyrah bin Shu´bah na Abu Sufyaan bin Harb kuliendea al-Laat katika mji wa at-Twaaif na akawaamrisha waliangamize. Vivyo hivyo akamtuma Khaalid bin al-Waliyd kuliendea al-´Uzzaa na kulivunja, akaukata mti na akaliua jini la kike lililokuwa likizungumza na watu ili kuwapoteza. Vilevile akamtuma ´Aliy bin Abiy Twaalib kuliendea Manaat akalivunja na kulitokomeza[1].

Ikiwa masanamu haya yalishindwa kujiokoa yenyewe, ni vipi yangeliweza kuwaokoa watu wake na wale wenye kuyaabudu?

أَفَرَأَيْتُمُ اللَّاتَ وَالْعُزَّىٰ وَمَنَاةَ الثَّالِثَةَ الْأُخْرَىٰ

“Je, mmeona al-Laat na al-‘Uzzaa na Manaat mwengine wa tatu?”

Yalienda wapi? Yalikunufaisheni? Je, yaliweza kujitetea kutokamana na maaskari wa Allaah na majeshi ya wapwekeshaji?

Hii ni dalili yenye kuthibitisha kwamba kuna watu wenye kuabudu miti na mawe. Masanamu haya matatu ndio yalikuwa makubwa lakini pamoja na hivyo Allaah alitokomeza uwepo wake. Hayakuweza kujitetea yenyewe na wala hayakuweza kuwanufaisha watu wake. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwapiga vita pasi na kuzuiwa na masanamu yao. Haya ndiyo yaliyotajwa na Shaykh (Rahimahu Allaah) ili kuthibitisha kuwa kuna ambao walikuwa wakiabudu mawe na miti. Ametakasika Allaah kutokamana na mapngufu! Ni vipi watu wenye busara wanaweza kuabudu miti na mawe vitu visivyokuwa na uhai, akili na wala havitikisiki? Iko wapi akili ya mwanaadamu? Ametakasika Allaah na yale wanayoyasema kutakasika kukubwa!

[1] Tazama “Zaad-il-Ma´aad” (04/413-415).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Qawaa´id al-Arba´ah, uk. 29-31
  • Imechapishwa: 18/08/2022