11. Kulingana kwa Allaah juu ya ´Arshi Yake


Neno Istiwaa´ kilugha linaweza kuwa na maana nyingi ambazo zote zinazunguka juu ya ukamilifu na utimilfiu. Limetajwa katika Qur-aan kwa njia tatu:

Ya kwanza: Isiyofungamanishwa. Mfano wa maneno ya Allaah (Ta´ala):

وَلَمَّا بَلَغَ أَشُدَّهُ وَاسْتَوَى

 “Pindi [Muusa] alipofikia umri wa kupevuka na akakamilika sawasawa… “[1]

Ya pili: Iliyofungamanishwa na ilaa. Mfano wa maneno ya Allaah (Ta´ala):

ثُمَّ اسْتَوَى إِلَى السَّمَاء فَسَوَّاهُنَّ سَبْعَ سَمَاوَاتٍ

“Kisha Akalingana ilaa mbingu na akazifanya timilifu mbingu saba.”[2]

Bi maana akakusudia kwa matakwa kamilifu.

Ya tatu: Iliyofungamanishwa na ´alaa. Mfano wa maneno ya Allaah (Ta´ala):

لِتَسْتَوُوا عَلَى ظُهُورِهِ

”Ili mlingamane sawasawa juu ya mgongo wake… “[3]

Bi maana ujuu na kuthibiti.

Allaah (Ta´ala) kulingana (Istiwaa) juu ya ´Arshi maana yake ni kuwa juu na kuthibiti juu yake kwa njia inayolingana na utukufu na ukubwa Wake. Kulingana ni sifa Yake ya kimatendo iliyothibitishwa na Qur-aan, Sunnah na maafikiano. Kuhusiana na Qur-aan, Allaah (Ta´ala) amesema:

الرَّحْمَنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَى

“Mwingi wa Rahmah amelingana juu ya ´Arshi.”[4]

Kuhusu Sunnah, al-Khallaal amepokea katika “as-Sunnah”, kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh kwa masharti ya al-Bukhaariy, kutoka kwa Qataadah bin Nu´maan (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia kuwa amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Baada ya Allaah kumaliza viumbe Vyake, alilingana juu ya ´Arshi.”[5]

Shaykh ´Abdul-Qaadir al-Jaylaaniy amesema:

“Imetajwa katika kila Kitabu ambacho Allaah amemteremshia kila Mtume.”[6]

Ahl-us-Sunnah wameafikiana juu ya kwamba Allaah (Ta´ala) yuko juu ya ´Arshi Yake. Hakuna yeyote katika wao aliyesema kuwa hayuko juu ya ´Arshi Yake. Ni jambo lisilowezekana kunukuu hilo kutoka kwao; si kwa andiko wala kidhahiri.

Kuna mtu alimwambia Imaam Maalik (Rahimahu Allaah):

“Ee Abu ´Abdillaah!

الرَّحْمَنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَى

“Mwingi wa Rahmah amelingana juu ya ´Arshi.”

Amelingana vipi?” Maalik akainamisha kichwa chake mpaka kijasho kikamtoka. Halafu akasema: “Kulingana kunajulikana. Namna haijulikani. Kuamini hilo ni wajibu. Kuulizia hilo ni Bid´ah. Sikuoni vyengine zaidi ya kuwa ni mtu wa Bid´ah.” Baada ya hapo akaamrisha atolewe nje[7].

Mfano wa hayo yamepokelewa kutoka kwa mwalimu wa Maalik Rabiy´ah bin Abiy ´Abdir-Rahmaan[8].

Maneno yake “Kulingana kunajulikana” bi maana kilugha. Maana yake ni ujuu na kuthibiti.

Maneno yake “Namna haijulikani” ina maana kwamba hatuwezi kuelewa namna ambavyo Allaah (Ta´ala) amelingana juu ya ´Arshi Yake kwa akili zetu. Njia pekee ya kuelewa hilo ni kwa njia ya Wahy, jambo ambalo Wahy haukulitaja. Ikiwa hakuna dalili yoyote ya hilo kiakili wala Wahy, namna itabaki kuwa haijulikani. Hivyo ni ni lazima kulinyamazia.

Maneno yake “Kuamini hilo ni wajibu” maana yake ni kwamba ni wajibu kuamini kuwa Allaah amelingana juu ya ´Arshi Yake kwa njia inayolingana Naye. Kwa sababu Allaah amejielezea hilo Mwenyewe na ndio maana ni wajibu kuthibitisha hilo na kuliamini.

Maneno yake “Kuulizia hilo ni Bid´ah” maana yake ni kwamba kuuliza kuhusu namna ya Kulingana ni Bid´ah. Hilo ni kwa sababu suala hili halikuwa lenye kujulikana wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala wakati wa Maswahabah zake.

Haya aliyosema Imaam Maalik (Rahimahu Allaah) kuhusu Kulingana ndio mzani unaotumika katika sifa zote ambazo Allaah (Ta´ala) amejithibitishia Mwenyewe katika Kitabu Chake na ambazo Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemthibishia. Tunajua maana yake na wala hatujui namna yake kwa vile Allaah ndiye ametueleza nazo na wala hakutueleza namna yazo. Kuzungumzia sifa ni sehemu ya kuzungumzia dhati. Ikiwa tunamthibitishia Allaah (Ta´ala) kuwa na dhati bila ya kuifanyia namna, kadhalika tunamthibitishia sifa Zake bila ya kuzifanyia namna.

Baadhi ya wanachuoni wamesema:

“Mtu Jahmiy akikwambia: “Allaah anashuka katika mbingu ya dunia. Hushuka namna gani?” Mwambie: “Allaah ametueleza kuwa anashuka na wala hakutueleza namna anavyoshuka.”

Wengine wakasema:

“Mtu Jahmiy akikuuliza ni namna gani sifa ya Allaah ilivyo, mjibu: “Dhati Yake iko vipi?” Hatoweza kuifanyia namna dhati ya Allaah. Hivyo umwambie: “Ikiwa huwezi kuifanyia namna dhati Yake, vilevile mtu hawezi pia kuifanyia namna sifa Yake kwa sababu sifa ni za Yule mwenye kusifika nazo.”

Mtu akisema:

“Ikiwa kulingana kwa Allaah juu ya ´Arshi Yake maana yake ni kuwa juu yake, basi hiyo ina maana Allaah atakuwa ni mkubwa, mdogo au atakuwa analingana na ´Arshi. Hili linapelekea Allaah kuwa yuko na kiwiliwili, jambo ambalo Allaah hawezi kusifika nalo.”

Ni jambo lisilo na shaka kuwa Allaah ni mkubwa kuliko ´Arshi na kuliko kila kitu. Hata hivyo halilazimishi kitu katika malazimisho batilifu ambayo Allaah ametakasika nayo.

Kuhusu maneno kwamba ni jambo lisilowezekana kabisa Allaah kusifika kuwa na kiwiliwili, uzungumziaji wa kiwiliwili ambao haukufungamanishwa, sawa iwe kwa njia ya kuthibitisha au kukanusha, ni jambo la Bid´ah ambalo halikuthibiti si katika Qur-aan, Sunnah na maneno ya Salaf. Ni katika maneno ya kijumla yanayohitajia ufafanuzi:

Kwa kusema kiwiliwili ikiwa kunakusudiwa kitu kilichoumbwa na kutengenezwa na ambacho kiungo kimoja cha mwili kinahitajia kingine, hili ni jambo lisilowezekana akasifiwa Allaah, Aliye hai, Mwenye kusimamia mambo yote.

Kwa kusema kiwiliwili ikiwa kunakusudiwa kilichosimama kivyake na kinasifika kwa njia inayolingana Naye, ni jambo lenye kuwezekana kwa Allaah (Ta´ala). Allaah yuko kivyake na anasifika na sifa kamilifu zinazolingana Naye (Subhaanahu wa Ta´ala).

Lakini ilipokuwa neno “kiwiliwili” linaweza kufahamika kwa njia ya haki na batili kwa nisba ya Allaah, mtu asikanushe wala kuthibitisha hilo kwa njia isiyofungamanishwa.

Malazimisho haya yanayosemwa na Ahl-ul-Bid´ah kwa lengo la kufikia kukanusha zile sifa kamilifu ambazo Allaah amejisifia nazo ziko namna mbili:

Ya kwanza: Malazimisho sahihi ambayo hayapingani na ule ukamilifu ambao ni lazima kwa Allaah kusifika nao. Aina hii ni sahihi na ni wajibu kuizingatia. Vilevile ni wajibu kubainisha kuwa ni jambo linalowezekana kwa nisba ya Allaah.

Ya pili: Malazimisho batilifu ambayo yanapingana na ule ukamilifu ambao ni lazima kwa Allaah kusifika nao. Aina hii ni batili na ni wajibu kuikataa. Vilevile ni wajibu kubainisha kuwa hayalazimishi kitu kabisa katika maandiko ya Qur-aan na Sunnah. Kwa sababu Qur-aan na Sunnah ni haki na maana zake ni haki na haki haiwezi kulazimisha kitu cha batili kabisa.

Mtu akisema:

“Mkisema kuwa Allaah amelingana juu ya ´Arshi Yake, mtu anaweza kufikiria kuwa ni Mwenye kuihitajia ili iweze kumbeba.”

Kila anayejua ukubwa wa Allaah (Ta´ala) na uwezo Wake mkamilifu, nguvu na ukwasi Wake, haiwezi kumwingia akilini mwake akafikiria kuwa Allaah ni Mwenye kuhitajia ´Arshi Yake ili iweze kumbeba. Itawezekanaje ilihali ´Arshi na vinginevyo vyote ni vyenye kunyenyekea/kumuhitajia Allaah? Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ تَقُومَ السَّمَاءُ وَالْأَرْضُ بِأَمْرِهِ

“Katika alama Zake ni kwamba mbingu na ardhi zimesimama kwa amri Yake.”[9]

Mtu akiuliza kama ni sahihi kufasiri kulingana kwa Allaah juu ya ´Arshi kwamba ni kutawala juu ya ´Arshi, kama walivyofasiri Mu´attwilah ili kukimbia malazimisho haya. Tafsiri hii ni ya kimakosa kutokana na sababu zifuatazo:

Ya kwanza: Hata kama malazimisho haya yangelikuwa ni ya sahihi, haina maana kuwa haiwezi kufasiriwa kwa maana yake ya kihakika. Yangelikuwa batili, basi isingewezekana maandiko ya Qur-aan na Sunnah yakawa na malazimisho ya batili. Mwenye kufikiria hivo ni mpotevu.

Ya pili: Aayah kufasiriwa kuwa ni kutawala kunalazimisha malazimisho batili yasiyokwepeka. Moja wapo ni kuwa yanapingana na maafikiano ya Salaf. Jengine ni kwamba itafaa kusema kuwa Allaah amelingana juu ya ardhi na mengineyo ambayo Allaah ametakasika nayo. Lazimisho la tatu ni kuwa Allaah (Ta´ala) asingelikuwa na utawala juu ya ´Arshi isipokuwa baada ya Yeye kuumba mbingu na ardhi.

Ya tatu: Aayah kufasiriwa kuwa ni kutawala ni jambo lisilojulikana katika lugha ya kiarabu. Bali ni kuisemea uongo lugha. Qur-aan imeteremshwa kwa lugha ya kiarabu na hivyo hatuwezi kuifasiri kwa njia ambayo waarabu hawaitambui.

Ya nne: Wale wenye kusema kuwa maana yake ni kutawala wamekubali kuwa hii ni maana ya kimajazi/kimafumbo. Maana ya kimajazi haikubaliwi isipokuwa baada ya kutimia masharti mane:

Mosi: Dalili sahihi yenye kupelekea kuliondosha tamko kutoka katika udhahiri wake na kulipeleka katika maana ya majazi.

Pili: Kuwepo uwezekano wa kilugha ya kwamba maana ya kimajazi kweli inafahamika kwa njia hiyo.

Tatu: Kuwepo uwezekano wa maana ya kimajazi inaendana na mtiriri huo wa kimaana. Haihitajii kuendana na mitazamo yote kwa sababu ya vizuizi vingine.

Nne: Dalili ibainishe kuwa uelewa kweli unatakiwa uwe majazi kwa vile tamko linaweza kuwa na uelewa mwingine. Ndio maana ni lazima kuwepo dalili ya uanishaji – na Allaah ndiye anajua zaidi.

[1] 18:14

[2] 02:29

[3] 43:13

[4] 20:05

[5] Ibn-ul-Qayyim ameitaja katika ”Ijtimaa´-ul-Juyuush al-Islaamiyyah”, uk. 34.

[6] al-Ghunyah, uk. 96.

[7] Tazama ”Siyar A´laam-in-Nubalaa’” (8/100) na ”al-Asmaa’ was-Swifaat” ya al-Bayhaqiy (515). Haafidhw Ibn Hajar amesema katika ”Fath-ul-Baariy” (13/407) ya kwamba mlolongo wa wapokezi wake ni mzuri.

[8] Tazama ”al-Asmaa’ was-Swifaat” (516).

[9] 30:25

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyah, uk. 40-44
  • Imechapishwa: 14/01/2020