11. Kufaa kwa wanandoa kuoga pamoja

9- Wanandoa kuoga pamoja

Inajuzu kwao wanandoa wawili kuoga sehemu moja hata kama mwanaume atamuona mwanamke na mwanamke akamuona mwanaume. Kumekuja Hadiyth juu ya hilo:

1- ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia akisema:

“Mimi na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) tulikuwa tukioga kwenye chombo kimoja kilichokuwa kati yangu mimi na yeye kiasi cha kwamba mikono yetu ilikuwa ikipishana ndani yacho. Akishindana nami mpaka nafikia kusema: “Nibakishie [maji], nibakishi.” Tulikuwa katika hali ya janaba.”[1]

2- Mu´aawiyah bin Haydah amesimulia:

“Nilisema: “Ee Mtume wa Allaah! Sehemu zipi za siri zinatakiwa kuonekana na ni zipi tunatakiwa kuhadhari nazo?” Akasema: “Hifadhi sehemu zako za siri isipokuwa mbele ya mke wako au yule ambaye amemilikiwa na mikono yako ya kuume[2].” Nikasema: “Ee Mtume wa Allaah! Vipi ikiwa jamaa wako wao kwa wao?” Akasema: “Ikiwa utahakikisha hakuna yeyote atakayeona tupu zenu, basi fanya hivo.” Nikasema: “Ee Mtume wa Allaah! Vipi ikiwa mmoja wetu yuko uchi?” Akasema: “Allaah anastahiki zaidi kuonewa hawa kuliko watu wengine.”[3]

[1] Ameipokea al-Bukhaariy, Muslim, Abu ´Awaanah katika “as-Swahiyh” zao na siyaaq ni ya Muslim na nyongeza ni ya kwake.

[2] Ibn ´Urwah al-Hanbaliy amesema:

“Inaruhusiwa kwa kila mmoja katika wanandoa kutazama mwili mzima wa mwenzie na kuupapasa kukiwemo tupu kutokana na Hadiyth hii. Jengine ni kwa sababu ni halali kwake mume kustarehe na tupu na hivyo itakuwa inafaa kwake mume kuitazama na kuipapasa kama viungo vyengine vya mwili.”

Haya ndio madhehebu ya Maalik na wengineo. Ibn Sa´d amepokea kutoka kwa al-Waaqidiy ambaye amesema:

“Nilimuona Maalik bin Anas na Ibn Abiy Dha´ib hawaoni ubaya kwa mume kumtazama mke na mke kumtazama mume.”

Kisha ´Urwah akasema:

“Imechukizwa kutazama tupu. Hakika ´Aaishah amesema: “Sikuwahi kuona tupu ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

Mlolongo wa wapokezi wake ambao ni dhaifu ulifichikana kwake, jambo ambalo limetangulia kulitaja.

[3] Wameipokea waandishi wa “as-Sunan” isipokuwa an-Nasaa´iy ambaye ameipokea katika “al-´Asharah” (01/76) na wengineo.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Aadaab-uz-Zafaaf, uk. 109-113
  • Imechapishwa: 08/03/2018