11. Kitu cha kwanza kinachotakiwa kupewa kipaumbele


Tawhiyd ndio msingi wa dini yote. Maamrisho, makatazo, ´ibaadah na utiifu wote umejengwa juu ya Tawhiyd yenye maana ya kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhamamd ni Mtume wa Allaah. Shahaadah mbili ambazo ndio nguzo ya kwanza ya Uislamu. Matendo wala ´ibaadah hayasihi na kukubaliwa pasi na Tawhiyd. Hakuna yeyote atakayesalimika kutokamana na Moto na kuingia Peponi pasi na Tawhiyd na ´Aqiydah sahihi.

Kwa ajili hiyo ndio maana wanachuoni wakatilia umuhimu mkubwa suala la Tawhiyd. Kwa sababu Allaah aliwatumiliza Mitume na akateremsha Vitabu kwa ajili ya Tawhiyd. Kisha baada ya kutimia kwa Tawhiyd ndio mtu atatakiwa matendo mengine. Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipomtuma Mu´aadh (Radhiya Allaahu ´anh) kwenda Yemen alimwambia:

“Hakika wewe unawaendea watu katika watu wa Kitabu. Hivyo basi iwe kitu cha kwanza utakachowalingania kwacho iwe ni kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah. Ikiwa watakutii kwa hilo, basi wafundishe ya kwamba Allaah amewafaradhishia swalah tano kila mchana na usiku. Ikiwa watakutii kwa hilo, wafundishe ya kwamba Allaah amewafaradhisha zakaah itayochukuliwa kutoka kwa matajiri wao na wapewe mafakiri wao. Ikiwa watakutii kwa hilo, tahadhari na kuwachukulia mali yao. Iogope du´aa ya mwenye kudhulumiwa, kwani hakika hakuna baina yake na baina ya Allaah kizuizi.”[1]

Kinacholengwa ni pale aliposema:

“Hivyo basi iwe kitu cha kwanza utakachowalingania kwacho iwe ni kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah.”

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Nimeamrishwa kuwapiga watu vita mpaka washuhudie ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah. Wakiyasema basi imesalimika kwangu damu na mali yao, isipokuwa kwa haki yake – na hesabu yao iko kwa Allaah (´Azza wa Jall).”[2]

Hii ni dalili inayofahamisha kwamba Tawhiyd ndio msingi unaopaswa kupewa kipaumbele kabla ya kila kitu kingine. Kisha baada ya hapo ndio kunakuja mambo mengine ya dini na ´ibaadah. Kwa ajili hiyo kama tulivosema ndio maana wanachuoni wakatilia umuhimu mkubwa maudhui haya na wakatunga tungo nyingi, vilivyoongelea kwa ufupi na kwa undani, wakavipa majina kwa mujibu wa maudhui na I´tiqaad.

Miongoni mwa vitabu hivyo ni kitabu hiki kilicho mbele yetu, nacho ni “Kitaab-ut-Tawhiyd” cha Shaykh-ul-Islaam na Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) katika karne ya kumi na mbili. Kitabu hiki ni miongoni mwa vitabu bora vilivyoandikwa kuhusu Tawhiyd kwa sababu kimejengwa juu ya Qur-aan na Sunnah. Kwa sababu katika kila mlango mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) hutaja Aayah muhimu za Qur-aan, Hadiyth ambazo ima ni Swahiyh inapokuja katika cheni za wapokezi au maana na maneno ya maimamu waliobainisha maana ya Aayah na Hadiyth hizi. Kwa msemo mwingine kitabu hiki hakikujengwa juu ya soga za watu au maneno kutoka kwa mwandishi mwenyewe. Bali kitabu chote kimejengwa juu ya maneno ya Allaah, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na maneno ya maimamu waliotangulia. Hilo lenyewe linathibitisha umuhimu wa kitabu hiki. Hivyo hakitokamani na maneno ya fulani wala maneno ya Ibn ´Abdil-Wahhaab. Kitabu kimejengwa juu ya maneno ya Allaah, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na maneno ya maimamu. Hivi ndivo zinatakiwa kuwa tungo.

[1] al-Bukhaariy (1395) na Muslim (19).

[2] al-Bukhaariy (6924), Muslim (124) na Ahmad (67).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: I´aanat-ul-Mustafiyd bi Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 17-18
  • Imechapishwa: 11/09/2019